DKT. MWINYI: ZANZIBAR IPO HATUA MPYA KATIKA MAGEUZI YA KIUCHUMI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imeingia katika hatua mpya ya mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuimarisha ushindani katika soko la kimataifa kwa kupanua fursa za uwekezaji, kuimarisha msingi mpana wa uchumi na kujenga mazingira rafiki yatakayowezesha ukuaji endelevu na ustawi wa wananchi.
Ameeleza kuwa Zanzibar inaendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi kwa vitendo kupitia dira iliyo wazi ya mabadiliko endelevu, kufungua milango kwa wawekezaji na kuimarisha mazingira ya uwekezaji. Amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, bandari, uzalishaji wa umeme, maendeleo ya utalii na huduma za umma, sambamba na kufanya mageuzi ya kitaasisi yanayolenga kuimarisha sekta ya uwekezaji.
Rais Dkt. Mwinyi amesema imani ya wawekezaji haijengwi na maendeleo ya miundombinu pekee, bali pia inategemea kuwepo kwa usalama, utulivu, mazingira ya biashara yanayotabirika na usimamizi madhubuti wa sheria. Amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali, kuboresha usimamizi wa ardhi, kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili kurahisisha uwekezaji na kuifanya Zanzibar kuwa nchi yenye ushindani zaidi katika soko la kimataifa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema zaidi ya miradi 800 ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 9 inaendelea kutekelezwa Zanzibar, huku ZIPA ikiendelea kurahisisha huduma muhimu za uwekezaji kupitia mfumo mmoja ili kupunguza urasimu na kuongeza ufanisi katika uanzishaji wa biashara
Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inatoa fursa kwa wawekezaji wa kigeni kumiliki kampuni kwa asilimia 100 na kusajili biashara zao bila kulazimika kuingia ubia na wazawa, pamoja na kuhamisha faida ya biashara nje ya nchi. Amesema hatua hiyo inadhihirisha dhamira ya Serikali ya kujenga mazingira rafiki, salama na yenye ushindani kwa wawekezaji wa kimataifa.
Ameongeza kuwa uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 7.3, huku mfumuko wa bei ukidhibitiwa kwa takribani asilimia 4.1, hali inayoonesha kuimarika kwa sekta mbalimbali pamoja na usimamizi mzuri wa uchumi.
Mapema baada ya kuwasili katika ukumbi wa mkutano huo, Rais Dkt. Mwinyi alitembelea maonesho ya taasisi za uwekezaji na wafanyabiashara yaliyofanyika pembezoni mwa Jukwaa la Uwekezaji Zanzibar 2026, ambapo alijionea bidhaa, huduma na fursa mbalimbali za uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano ya Awali ya Ushirikiano baina ya Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji wa Maeneo Huru Zanzibar (ZIPA) na Taasisi ya Wawekezaji ya Marekani, pamoja na mkataba wa pili wa ushirikiano kati ya ZIPA na Benki ya AfriExim.












Comments
Post a Comment