MBETO: MELI YA KWANZA YA MAFUTA ZANZIBAR NI UTEKELEZAJI ILANI YA CCM 2025/2030
KUTIA Nanga Meli ya kwanza kubwa ya Kimataifa yenye lita Milioni 36 za Mafuta katika Bandari Jumuishi Mangapwani, Zanzibar ni sehemu ya ahadi iliyopo kwenye vipaumbele takribani 10 katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu uliopita 2025 na ni maono ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuifanya Zanzibar kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta.
Akizungumzia mjini Unguja 03 Juni 2026 kuhusiana na kuwasili kwa meli hiyo kubwa ya Kimataifa kwa mara ya kwanza toka Zanzibar iwepo, Katibu wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema lengo ni kuwa na akiba ya miezi mitatu hadi minne.
"Tunaendelea na ujenzi wa hifadhi kubwa ya mafuta Mangapwani na tayari makampuni yapo kule" alisema Mbeto.
Alibainisha kuwa mafuta ni muhimu katika Zanzibar inayokua kiuchumi kwa sasa na pia katika maisha ya kawaida ya wananchi kwani yakiwepo ya kutosha yanasaidia udhibiti wa kupanda kwa gharama za usafiri na usafirishaji hivyo kuzuia mfumuko wa bei za bidhaa na vyakula kwa wananchi.
"Serikali ya CCM imeahidi kuwaondolea wananchi wake changamoto mbalimbali ikiwemo ya upatikanaji wa mafuta kuwarahisishia shughuli zao za kila siku" alisema na kuongeza kuwa Dkt. Hussein Mwinyi ni Rais mwenye maono makubwa anayotekeleza kwa vitendo.
Meli hiyo kubwa yenye lita Milioni 36 za mafuta kutoka nchini, Saudi Arabia iliwasili na kuanza kushusha mwishoni mwa wiki iliyopita na kulingana na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kirangi kiasi hicho mafuta kinatosheleza takribani mwezi mmoja na kuanza kuwasili kwa meli hizo moja kwa moja ni hatua kubwa katika maendeleo na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Comments
Post a Comment