MBETO AHOJI ACT WAZALENDO KUPEWA ARDHI BARA, KUTIBIWA MUHIMBILI
KATIBU wa Kamati Maalum NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amewataka viongozi wa ACT Wazalendo wakavisome vizuri vifungu vya Katiba wanavyodai kuwa suala la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) si la Muungano hivyo vijana wa Zanzibar hawapaswi kujiunga nalo.
Pia wajiulize iwapo suala la Afya na Ardhi kama nayo yapo kwenye Muungano na kuwataka kushughulika na mambo ya msingi na sio kutaka kuwanyima vijana wa Zanzibar fursa zitokanazo na JKT kwani suala hilo ni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anashangaa uwezo wa wanasheria wa chama hicho kulijua hilo.
Alibainisha Mwenezi Mbeto kuwa Katiba Kifungu namba 147 inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaunda Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1975 yanaifanya JKT ambayo inaundwa na Kifungu Sheria namba 16 cha Jeshi la Kujitolea Kutumikia Taifa (National Service Act.) 1964, inafanywa kijeshi kuwa Kamandi ya JWTZ.
Mbeto kuwa kutokana na muundo huo wa kikatiba, JWTZ ni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na JKT ni Kamandi iliyo ndani ya JWTZ, hivyo kudai vingine kunashangaza.
"Pale wapo na wanasheria chungu zima (wengi) lakini inashangaza" alisema Mbeto ambaye idara yake pamoja na mambo mengine, inahusika na elimu, itikadi na mafunzo ndani ya CCM.
Alisema mwenezi huyo kuwa vijana wa upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wasinyimwe kutumia fursa za JKT.
"Mbona wanapewa ardhi Bara hawasemi? Mboma tunapewa rufaa tunakimbilia Muhimbili kwani hayo hapo kwenye Muungano?" alihoji Mbeto.
Mwenezi huyo alisema wajiulize pia mbona askari toka Zanzibar walipigana vita Uganda na makumi ya watoto wao wanaomba nafasi za ajira zikitangazwa Polisi, Uhamiaji, JWTZ na majeshi mengine.
"Wakati ukifika hatutulii maofisini wanakuja Oooh, mwanangu kaomba nisaidie" alisema na kuongeza kuwa kuna mambo mengi ya maendeleo ya kujadili sio kila siku kuzua yasiyo na msingi.
Mbeto alisema kuwa madai kuwa watoto wao watavuliwa Hijjab hayana msingi kwani jeshi lina mfumo wake ndio maana jeshini wote ni askari hakuna wa kike au kiume na linapokuja suala la imani ndio maana nchi zingine wanawake hawaruhuxiwi jeshini.
Alishangaa hayo kusemwa JKT wakati hata Zanzibar wanapoomba zinapotokea nafasi kujiunga na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi (SMZ), vya KMKM, Uhamiaji, Polisi, JKU, KVD hilo hawahoji.
"Vikosini, wananyoa nywele na kubaki na vipara, wanavaa sare za miçhezo kama mafunzo ya kijeshi yanavyotaka?" aliuliza.
Chama ACT Wazalendo ambacho hadi sasa hakijajiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar ili kuwatumikia waliowaowapigia kura, kimetakiwa kujua msingi mkuu wa mafunzo ya JKT.
Alitanabaisha Mwenezi Mbeto kuwa JKT ni kuwajengea vijana uzalendo, mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya ulinzi wa Taifa lao, kujitolea kulitumikia Taifa na mafunzo ya stadi mbalimbali ambazo zinaenda kuwajengea kujitegemea.

Comments
Post a Comment