DKT. MWINYI AKARIBISHA WAFANYABIASHARA TOKA UARABUNI KUWEKEZA ZANZIBAR


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchi za Kiarabu kuwekeza Zanzibar, akibainisha kuwa kuna mazingira bora na fursa nyingi katika sekta mbalimbali.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, 05 Juni 2026, Ikulu Zanzibar, alipokutana na Mabalozi wa nchi za Kiarabu wanaoziwakilisha nchi zao nchini Tanzania, waliofika kwa ajili ya kumsalimia pamoja na kumpongeza kwa hatua kubwa ya maendeleo inayofikiwa na Zanzibar hivi sasa.

Rais Dkt. Mwinyi amezipongeza nchi hizo za Kiarabu kwa kuimarisha na kuendeleza uhusiano wake na Tanzania, ikiwemo Zanzibar, pamoja na misaada yao katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ambayo ameielezea kuwa ni kichocheo muhimu cha maendeleo, ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na ushirikiano.

 Dkt. Mwinyi amewahakikishia kuwa Zanzibar inathamini misaada inayotolewa na nchi hizo katika sekta za elimu, afya na miundombinu, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kihistoria na wa muda mrefu baina ya mataifa hayo na Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amewashauri Mabalozi hao kuzitangaza fursa zilizopo Zanzibar kwa wawekezaji na wafanyabiashara katika nchi zao ili waje kuwekeza, hususan katika utalii na uchumi wa buluu.

Amesema Serikali imeandaa sera, mazingira mazuri ya uwekezaji na vivutio mbalimbali.

Alibainisha kuwa sekta ya utalii, ambayo ni nguzo muhimu ya uchumi wa Zanzibar na inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa, inaendelea kuwa na fursa za ushirikiano na uwekezaji ambazo wafanyabiashara kutoka mataifa hayo ya Kiarabu wanaweza kuzitumia kwa tija na mafanikio.

Akizungumzia uchumi wa buluu, amesema pia ni sekta muhimu yenye fursa nyingi, ikiwemo utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, utalii wa mikutano (MICE), uvuvi, utalii wa michezo, utalii wa fukwe, mazao ya baharini pamoja na fursa zilizopo katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani.

Rais Dkt. Mwinyi amezipongeza taasisi mbalimbali kutoka nchi za Kiarabu zinazoendelea kuwekeza na kuisaidia Zanzibar katika nyanja tofauti za maendeleo, uchumi na ustawi wa jamii na amezihakikishia ushirikiano zaidi, sambamba na kuyakaribisha makampuni katika sekta za biashara na uwekezaji.

Pia Rais Dkt. Mwinyi ameziomba nchi hizo kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi na mkakati wake wa kuleta mageuzi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa mfumo wa kidigitali, kuwajengea uwezo watu wake kupitia mafunzo katika nyanja mbalimbali za teknolojia, pamoja na kuongeza fursa za mafunzo kwa Wazanzibari katika nchi hizo za Kiarabu.

Mabalozi waliofika Ikulu na nchi zao katika mabano ni pamoja na Ahmada El Badaoui (Comoro), Balozi  Sharif Abdelhamid

 (Misri),Yahya Ahmed Okesh (Saudi Arabia) na Mohamed Abdala Mohamed Abdelhameed (Sudan), Ghalib Zemane (Algeria) na Salam Abuu Sharara (Palestine) 

Makaimu mabalozi wanaowakilisha zao nchini walio onana na Rais Dkt. Mwinyi ni Acram Fayz Alhada (Syria), Ahmad Sale Al Umar (Yemen), Abdul  

Saeed Al Naimi (Qatar), Abdillarif Abdullah Hilowle (Somalia) na Ezzedin Bahri (Libya).

Akiwasilisha salamu kwa niaba ya Mabalozi hao, Balozi wa Saudi Arabia, Yahya Ahmed Okesh, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake unaoleta maendeleo na mabadiliko makubwa katika uchumi wa Zanzibar na ustawi wa watu wake.

Aiidha, amesifu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ujenzi wa miundombinu, ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na bandari, pamoja na kuimarika kwa sekta ya utalii, hatua inayochochea kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaokuja Zanzibar.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA