UTALII WA MICHEZO KUWANUFAISHA KIUCHUMI WANAOZUNGUKA HIFADHI
Na Happiness Sam - Kitulo
UTALII wa michezo umeendelea kuwa chanzo kipya cha kuongeza mapato kwa jamii zinazozunguka Hifadhi za Taifa Tanzania.
Kadri shughuli hizi zinavyokua, wananchi wanaoishi karibu na hifadhi pamoja na wale wa mikoa jirani wameendelea kunufaika kwa kiwango kikubwa, hasa kupitia fursa za kiuchumi zinazotokana na ongezeko la wageni.
Hayo, yamejiri 02 Mei 2026 wakati wa mbio za Kitulo Garden Marathon ambapo wananchi kutoka maeneo ya jirani wamejitokeza kufanya biashara mbalimbali katika mbio hizo kitu ambacho kitawaongezea mapato na kuwaepusha na shughuli zisizo rasmi za kuingia na kufanya ujangili hifadhini.
Akitoa pongezi kwa washiriki wa mbio hizo, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Mafuru amesema mbali na utalii wa michezo uliofanyika, vile vile imeshuhudiwa wananchi wengi wakijipatia kipato kwa kuuza bidhaa na huduma mbalimbali kama zikiwemo za malazi, vyakula, vinywaji, kazi za mikono na huduma za usafiri hali hii inaonyesha kwamba utalii ni jumuishi.
"Hali hii inachagiza vitu vinne muhimu ambavyo ni ni 'unakimbia, unatangaza, unahifadhi lakini pia unasaidia kwa jamii' na vitu kama hivyo, vitaongeza ushiriki wa jamii katika kuhifadhi maliasili" alisema Mkurugenzi Mafuru.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TANAPA Godwell Ole Meing’ataki ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kusini alisema tukio hilo limefungua fursa kwa wajasiriamali na kuwafanya wananchi kutambua umuhimu wa hifadhi hiyo.
Vilevile Kamishna Meing’ataki aliongeza kuwa kiingilio walichotoa washiriki hao zaidi ya 300 kimeongeza mapato kwa serikali na kukuza uchumi, fedha ambazo zitatumiwa na serikali katika kuimarisha sekta mbalimbali nchini.
Kitulo Garden Marathon imehusisha mbio za kilomita 5, 10 na 21, zikivutia washiriki wengi na kuleta ushindani wenye tija.
Washindi wa mbio hizo walizawadiwa zawadi mbalimbali, huku washindi watatu wa kwanza kupewa fursa ya kulala na kutalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kitulo pamoja na wenza wao kwa muda wa siku mbili.









Comments
Post a Comment