UJIO WA KAGAME, RUTTO AIBU KWA MAKUWADI WA KISIASA E.A-MBETO
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetaja ziara za Rais wa Rwanda na wa Kenya nchini ni majibu tosha kwa wanasiasa na wanaharakati kiliowaita uchwara, wanaojihusisha na ukuwadi wa kisiasa Afrika Mashariki.
Hivyo basi, CCM kimewataka wana Afrika Mashariki wote kupuuza uvumi usio na mashiko ukidai Mataifa E.A hayana uhusiano Mwema.
Matamshi hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis ofisini kwake Kisiwandui Visiwani Zanzibar.
Mbeto alieleza hayo mara baada ya Marais hao kuitembelea nchi huku akieleza kuwa uhusiano wa Tanzania kidiplomasia wa Kikanda na Kimataifa, hautadhoofika.
Mbeto alisema wapo baadhi ya wanasiasa na wanaharakati uhwara E.A ambao uelewa wao ni hafifu katika Uongozi, siasa na utawala, hueneza taarifa hasi zikidai Tanzania haina Uhusiano mzuri na Nchi jirani.
Alisema Tanzania itaendelea kufuata kanuni, taratibu, misingi ya Uongozi, utawala wa sheria bila kukiuka kanuni za kidiplomasia na kwamba itaheshimu miiko na kanuni ili kudumisha umoja na ushirikiano.
"Wako wapi wanasiasa na Wanaharakati viherehere wakaanga sumu, chuki na uongo. Zara za Rais Paul Kagame na Dkt. William Rutto zimewatia aibu makuwadi wa kisiasa na wapika majungu Afrika Mashariki" alisema Mbeto.
Katibu Mwenezi huyp alisema Tanzania na jirani zake, washirika wa maendeleo, wawekezaji, Jumuiya ya Afrika Mashariki na,Jumuiya za kikanda na Mashirika ya Kimataifa, zitaendeleza ushirikiano usio na shaka.
"Mataifa yetu yatizame mbele na kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayotanua wigo wa ajira na uwekezaji.
Tungependa kuziona sekta za mawasiliano, usafiri na biashara zikiimarika Tanzania daima haitatikiswa na kelele wakaanga sumu " alieleza.
Pia Mbeto alisema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikifanyakazi kwa ushirikiano na nchi zote jirani , hivyo uchonganishi wenye lengo la kuchochea mitafaruku, idhibitiwe mapema kwa nguvu ya pamoja.
"Tusingoje hadi hatari ishamiri ndipo udhibiti ufanyike. Tulinde mipaka yetu kwa nguvu na sauti moja. Uchonganishi na Uchochezi udhibitiwe ili usidhoofishe umoja, amani na maendeleo" alisisitiza Mbeto.
Mwenezi huyo akizungumzia nafasi ya demokrasia, uwazi na Utawala bora, alisema wananchi wamepewa uwanja mpana wa ushiriki wa demokrasia inayozingatia nidhamu, miiko na utii wa sheria.
'Serikali zimetoa nafasi pana ya Utekelezaji wa demokrasia shirikishi na si demokrasia holela. Serikali zetu zinaheshimu sheria, uhuru wa Kijamii wenye mipaka kwa mujibu wa sheria na katiba " alisema Mbeto.

Comments
Post a Comment