TARURA YAWATOA HOFU WAKAZI UJENZI BARABARA HONDOGO-WILLIAM SHIJA
Na Joseph Zablon, Dar es Salaam
WAKALA wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), imewatoa hofu wananchi wa eneo la Hondogo Kata ya Kibamba na kuwaeleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 6.14 upo kama ulivyopangwa na ulisitishwa kutokana na mvua zilizokuwa zinaendelea kunyesha.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma, Catherine Sungura alisema kutokana na hali hiyo, Wakala wa Mfuko wa Barabara (TANROAD), uliwaagiza Wakandarasi wote kuhakikisha wana wanaimarisha na kuzitunza njia mbadala zipitike hata wakati wa mvua kubwa.
"Unajua huwezi kuweka lami wakati mvua inanyesha" alisema na kuongeza kuwa utekelezaji wa DMDP II unaendelea.
Alisema chini ya mpango huo zinajengwa barabara za lami, zege, uwekaji wa taa za barabarani na miundombinu ya maji taka chini ya Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II) unaogharamiwa na Benki ya Dunia (WB).
Baadhi ya wakazi wa Hondogo walionyesha wasiwasi kuhusiana na ujenzi huo kutokana mkandarasi kuondoka na vifaa vyake kutoka eneo la mradi mara tu baada ya uwekaji wa jiwe la msingi uliofanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kiTaifa, Wazo Mwang'onda 16 April 2026.
Sungura alibainisha kuwa Benki ya Dunia (WB), imetoa jumla ya TSh. Bilioni 517 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami na zege zenye urefu wa kilometa 250 na maboresho mengine kwa Jiji la Dar es Salaam.
Mkuu huyo wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TARURA, alisema kuwa ujenzi na maboresho hayo ya miundombinu ya barabara yanafanyika katika wilaya zote tano za mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo barabara hiyo ya Hondogo Kata ya Kibamba, wilaya ya Ubungo.



Comments
Post a Comment