TANZANIA YAWASILI BRAZAVILLE, MKUTANO MAGAVANA AfDB


                                         Na Mwandishi Wetu, Brazaville

WAZIRI wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa Omar akiwa na watendaji wengine wa Serikali, amewasili nchini Congo, Brazzaville, ambako watashiriki Mkutano Mkuu wa 61 wa mwaka 2026 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Pia na Mkutano Mkuu wa 52 wa Mwaka wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF), uliopangwa kufanyika kuanzia tarehe 25 hadi 29 mwaka 2026, katika Mji huo.

Waziri Balozi Omar, ambaye ni Gavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ameambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali ambaye pia katika Muundo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ni Gavana Mbadala wa Benki hiyo (Alternate Governor), Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Kamishna wa Fedha za Nje, Rished Bade.

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Brazzaville, Maya Maya, Balozi Omar na msafara wake alilakiwa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Said Juma Mshana.

Mkutano huo ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe 3,000 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo baadhi ya viongozi wa nchi, Wakuu wa Serikali za Afrika, Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu, washirika wa maendeleo, wawakilishi wa sekta binafsi, viongozi wa asasi za kiraia, wasomi, taasisi za utafiti, NGOs, na wadau wengine.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Kuhamasisha Ufadhili wa Maendeleo ya Afrika kwa Wingi katika Dunia Iliyogawanyika”. Kauli hii inasisitiza umuhimu wa kuziba pengo la kifedha linalokua kwa mahitaji ya maendeleo ya Afrika, hasa katika mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani yanayobadilika kwa kasi.

Mkutano pia utajadili masuala mtambuka kama mageuzi ya kidijitali, uimarishaji wa taasisi na utawala bora. Haya yote yanalingana na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi, Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, na Mikakati Miuu Mitano ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (High 5s).

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA