TANZÀNIA KINARA UZALISHAJI ASALI NCHI ZA SADC


                                   Na Mwandishi Wetu,  Tabora

SEKTA ya nyuki nchini imeendelea kukua na kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali katika nchi za Afrika Mashariki (EAC), ya pili kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na ya 14 duniani.

Mafanikio hayo yamechangia uzalishaji wa ajira pamoja na kukuza pato la kaya na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Tabora, 22 Mei 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema usimamizi mzuri wa sekta ya nyuki umeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la uzalishaji wa asali kutoka tani 33,861 hadi tani 75,000 pamoja na kuongezeka kwa ajira mpya 43,055, hususan kwa vijana.

Dkt. Kijaji amefafanua kuwa kupitia kampeni ya “Achia Shoka, Tundika Mzinga”, kiwango cha uzalishaji wa asali kimeongezeka kwa kiasi kikubwa. 

Amesema thamani ya asali iliyouzwa nje ya nchi imeongezeka kutoka TSh.Bilioni 11.4 mwaka 2024 hadi kufikia TSh.Bilioni 19.2 mwezi Machi 2025, hatua inayoashiria ukuaji wa sekta ya nyuki na kuwanufaisha Watanzania, hasa wale wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yaliongozwa na kauli mbiu ya “Uhifadhi wa Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Taifa Letu” ambayo inayokwenda sanjari na mipango ya Taifa ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na mikakati mingine yenye lengo la kuhakikisha Taifa linaendelea kuhifadhi maliasili zake ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula.

Amesisitiza kuwa ufugaji nyuki una mchango mkubwa katika uhifadhi wa misitu na wanyamapori, uchavushaji wa mimea, upatikanaji wa chakula, dawa pamoja na malighafi za viwandani.

Maadhimisho hayo yaliambatana na maonesho ya mazao mbalimbali ya nyuki, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kuchakata na kuzalisha asali.

Sambamba na hayo, Dkt. Kijaji alipata fursa ya kufungua karakana ya mbao katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, kugawa mizinga ya kisasa 600 kwa vikundi vya wafugaji nyuki kutoka halmashauri za Urambo na Kaliua pamoja na wafugaji nyuki kutoka Chama cha Wenye Ulemavu wa Kusikia, ikiwa ni sehemu ya kuleta manufaa kwa Watanzania wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi za misitu.

Aidha, aligawa majiko banifu 500 yanayotumia umeme kidogo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora amewataka wananchi kuacha kukata miti kwa ajili ya nishati ya mkaa hadi pale tathmini itakapofanyika ili kutoa mwongozo bora wa uvunaji endelevu wa miti kwa ajili ya mkaa.

Pia amewahimiza wananchi kujikita katika matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kulinda mazingira.

Upande mwingine, msanii wa Singeli Misso Misondo  alinogesha kilele hicho cha Siku ya Nyuki Duniani kwa kufanya onesho la aina yake lililoisisimua hadhira iliyokuwepo.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA