TANZANIA, AFRIKA KUSINI, BOTSWANA ZANG'ARA UTALII AFRIKA


Na Mwandishi Wetu, Alexandria, Misri

NCHI kadhaa za Afrika zimeonesha ukuaji mzuri katika sekta za utalii huku ikitarajiwa ukuaji huo kuendelea kwa kasi na kutoa mchango zaidi kwa uchumi na jamii, licha ya changamoto mbalimbali za Dunia.

Hayo yamo kwenye ripoti mpya ya Baraza la Utalii na Usafiri Duniani (WTTC) ijulikanayo kama “Travel and Tourism Economic Impact 2025,” iliyotambulishwa kwenye Mkutano wa Baraza hilo unaofanyika kwenye meli ya Kitalii ya Crystal Cruises ambayo leo Jumamosi Mei 9, 2026, imefika katika Bandari ya Alexandria nchini Misri.

“Ripoti hii inaonesha mchango wa sekta ya utalii kwa uchumi na maendeleo ya watu ni mkubwa ikilinganishwa na sekta nyingine hivyo Serikali mbalimbali duniani zinapaswa kuipa sekta hii kipaumbele.

“Kwa upande wa mchango kwenye GDP Duniani mwaka 2025, utalii umechangia kwa asilimia 10.3 sawa na mapato ya Dola za Kimarekani Trilioni 11.7 na ikitarajiwa kukua hadi Dola Trilioni 16 mwaka 2035 na ajira kutoka watu milioni 371 hadi milioni 471 mwaka 2035” alisema Mtendaji Mkuu wa WTTC, Gloria Guevara, akiitambulisha ripoti hiyo.

Kwa upande wa Tanzania, ripoti hiyo inaonesha nchi za Afrika Kusini (asilimia 7.7) na Tanzania (asilimia 7.4) zimeongoza Afrika kwa kupokea mitaji zaidi ya kiuwekezaji katika sekta ya utalii zikiwa juu ya wastani wa Dunia ambao ni asilimia 3.8.

Aidha, Afrika Kusini, Tanzania na Kenya zimefanya vyema katika eneo la mapato ya watalii kununua bidhaa na kuzisafirisha nje ya nchi (visitor exports).

                       

Akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania, Dkt. Hassan Abbasi aliyehudhuria Mkutano huo, Bi Gloria ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuongeza mchango wa sekta ya utalii kwa uchumi na ajira za Watanzania.

Awali wakichangia mada kuhusu Mchango wa Utalii Katika Wakati wa Changamoto Marais Wastaafu Mauricio Macri (Argentina, 2015-2019), Felipe Calderón (Mexico, 2006-2012) na Waziri Mkuu wa zamani wa Italia, Matteo Renzi (2014-2016), wameeleza jinsi awali Serikali zao zilivyoshindwa kuupa utalii kipaumbele kabla ya kubaini mchango wa sekta hiyo na kuifanya kuwa msingi wa uchumi wa serikali zao.

Walitumia muda huo kuwakumbusha viongozi wa sasa kuienzi sekta hiyo kwani ina mchango mkubwa huku wakiwataka watendaji walio chini ya viongozi wa kisiasa kushauri ipasavyo.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA