SERIKALI YAONGEZA UWEKEZAJI KWA WAKUNGA


                                    Na Aisha Swahibu, WAF - Kilimanjaro 

SERIKAĹI kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuendelea kuongeza uwekezaji katika mafunzo, ajira, motisha na mazingira ya kazi kwa wakunga kwa lengo la kuzidi kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wakinamama nchini.

_Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe akizungumza wakati wa maadhimisho hayo._

Hayo yamesema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe leo 2 Mei 2026 wakati akizungumza katika Maadhimisho ya siku ya Mkunga Duniani yaliyofanyika Mkoani Kilimanjaro. 

"Nitoe wito kwa wakunga wote nchini kuendelea kutoa huduma za afya kwa weledi, juhudi na kuzingatia maadili ya taaluma zao ili kuhakikisha usalama wa mama na mtoto unaimarika" alisema Dkt. Shekalaghe.

_Baadhi ya watu waliohudhuria maadhimisho hayo wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe._

Alosema, hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka maadili ya taaluma huku akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuwawajibisha watoa huduma watakaoenenda kinyume na viwango vinavyotakiwa ili kulinda hadhi ya taaluma na usalama wa wagonjwa.

Aidha, Dkt. Shekalaghe ameihimiza jamii kutumia vituo vya afya ili kupata huduma sahihi kutoka kwa wakunga wataalamu badala ya kujifungulia nyumbani bila uangalizi wa kitaalamu huku akihimiza ushirikiano kati ya jamii na watoa huduma.

Katika maadhimisho hayo  yaliyohusisha 'Wakunga Marathon 2026', alisema ushirikiano huo ni muhimu hasa wakati wa dharura kwani huongeza uwezekano wa kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Katika hatua nyingine, Dkt. Shekalaghe ameitaka jamii kuwaunga mkono wakunga kwa kuwaheshimu, kushirikiana nao na kuhakikisha wajawazito wanafikishwa sehemu za huduma mapema na kwa wakati.

“Serikali inatambua mchango wenu wakunga kwa kazi kubwa mnayoifanya, Tuzo aliyotunukiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 'Goalkeeper' kama kinara wa kupunguza vifo vya mama na mtoto, lakini pia kuchaguliwa kwake kuwa Kinara wa masuala ya mama na mtoto Afrika, dhahiri ni juhudi na utendaji kazi wenu bora, hivyo nawapongeza sana” alisema Dkt. Shekalaghe.

ilevile, Dkt. Shekalaghe amesisitiza kuwa, wadau wa sekta ya afya kushiriki kikamilifu katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na kuweka mazingira bora yatakayowawezesha wakunga kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

Akizungumzia Wakunga Marathon, Dkt. Shekalaghe amewapongeza washiriki kwa kutumia michezo kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya ya mama na mtoto, akisisitiza kuwa kuwawezesha wakunga ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA