SERIKALI, WADAU KUIMARISHA MIKAKATI UUGUZI, UKUNGA NCHINI
Na Zakayo Mosha, WAF - Dodoma
WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeandaa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Watumishi na wadau Ukunga na Uzazi, unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Mkutano huo unawahusisha wauguzi viongozi ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Hospitali ya Taifa, Hospitali za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali maalum, Waratibu wa Kanda na Mikoa wa huduma za Afya ya uzazi na mama na mtoto.
Pia Waratibu wa huduma za M-Mama ngazi za Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kujadili namna bora ya kuboresha huduma hizo kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Prof. Tumaini Nagu wakati akifungua mkutano huo Mei 20, 2026 Jijini Dodoma amewataka wauguzi viongozi kujua nafasi zao, kutoa elimu kwa wauguzi pamoja na kusimamia wodi.
"Nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoboresha utoaji wa huduma za Afya hapa nchini ikiwemo miundombinu, vitendea kazi na kujali maslahi ya watumishi wa taaluma ya uuguzi na ukunga," amesema Prof. Nagu.
Kufuatia uwekezaji huo, Prof. Nagu amewapongeza wauguzi hao kwa kuwahudumia wagonjwa na kuwa walimu, walezi, kutatua changamoto binafsi za wagonjwa na kuwataka kundelee na moyo huo huo kwakiwa Serikali inatambua juhudi hizo na itaendelea kuwajali na kuboresha mazingira ya kazi.
Ameongeza kuwa, ni matarajio ya Serikali kupitia mkutano huo kutoka na mikakati ya kuendelea kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa kwa kuzingatia maadili, nidhamu, Utu na staha.
Aidha, Prof. Nagu amesema kuwa malengo ya Serikali ya awamu ya Sita ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kushuka kutoka 104 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 70 kwa kila vizazi hai 100,000.
"Ili kufanikisha malengo haya kila muuguzi atimize wajibu wake na wale wachache wanaokiuka misingi ya maadili ya kazi mbadilike kabla ya kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma," amesema Prof. Nagu
Katika hatua nyingine, Prof. Nagu amewakumbusha wauguzi, wakunga na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Ebola ambao umegundulika katika Nchi Jirani za Kongo DRC pamoja na Uganda ambapo amesema Serikali ya Tanzania imechukua tahathari kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah amewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo katika Sekta ya Afya kwa jinsi wanavyounga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupunguza vifo vya Mama na mtoto hapa nchini.
"Juhudi hizi zimezaa matunda na Tanzania imepata mafanikio makubwa ambapo vifo vya watoto wanaozaliwa vimepungua kutoka 556 mwaka 2022 na kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 hapa nchini na kupelekea Mhe. Rais Dkt. Samia kupewa tuzo kutoka nchini Marekani kwa kutambua mchango wake," amesema Bi. Ziada





Comments
Post a Comment