SERIKALI: HATUNA MPANGO WA KUPELEKA WANYAMAPORI KWENYE KIMOMDO
WANANCHI wa Isela-Ndolezi Mkoani Songwe wametakiwa kuendelea na shughuli za maendeleo katika maeneo yao kwa kushirikiana kikamilifu na Serikali katika uendelezaji wa utalii Kimondo kilichopo kwenye eneo hilo kwa kuwa Serikali haina mpango wa kupanua eneo hilo na kupeleka wanyamapori.
Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande, katika kikao cha 28 Mkutano wa tatu wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akijibu swali la Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga aliyetaka kufamu mpango wa Serikali kuwalipa fidia Wananchi wa Kitongoji cha Isela - Ndolezi ili kupisha upanuzi wa eneo la Kimondo na kuleta wanyamapori.
“Baada ya uchambuzi wa kina wa eneo lililopo sasa, Serikali iliona ni busara kuliendeleza eneo hilo ili kuona tija yake kabla ya kuwa na mipango ya kutwaa maeneo ya jirani. Hivyo, kwa sasa Serikali haina mpango wa kupanua eneo hilo wala kuanzisha shughuli nyingine tofauti na zile zinazoendelea kwenye eneo hilo kwa sasa.” alisisistiza Mhe. Chande
Awali Mhe. Chande amebainisha kuwa kufikia Mwaka 1967 Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Malikale ilitangaza Kimondo cha Mbozi kuwa eneo la Urithi wa Taifa kwa Tangazo la Serikali Na 90.
Hivyo, Wizara ilikasimisha rasmi kituo cha Kimondo hicho kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia Tangazo la Serikali Na.631 la tarehe 14/08/2020 ili kuimarisha usimamizi, uendeshaji na uendelezaji wa eneo hilo kwa lengo la kukuza uhifadhi na utalii wa mikoa ya Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.

Comments
Post a Comment