RAIS DKT. MWINYI KUJUMUIKA SALA YA EID EL HAJJ, KESHO PEMBA
Na Mwandishi Wetu, Pemba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasili Pemba leo, 26 Mei 2026, kwa ajili ya kujumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Eid El-Hajj pamoja na Baraza la Idd linalotarajiwa kufanyika kesho.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Pemba, alipokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hadid Rashid Hadid.
Rais Dkt. Mwinyi pia ametoa mkono wa pole kwa familia ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, kufuatia kifo cha ndugu yake, Marehemu Bakari Omar Kaabi, aliyefariki jana.
Rais Dkt. Mwinyi alifika nyumbani kwa familia ya marehemu, Changaweni Mfikiwa, kutoa mkono wa pole kwa Mufti Mkuu huyo wa Zanzibar, ndugu na jamaa, huku akiwasihi kuwa na ustahamilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa kuondokewa na mpendwa wao.
Marehemu Bakari Omar Kaabi amefariki jana tarehe: 25 Mei 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Abdalla Mzee, Mkoani, Pemba, na kuzikwa Ukutini. Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi. Amina.





Comments
Post a Comment