RAIS DKT. MWINYI APANDISHA KIMA CHA MSHAHARA ZANZIBAR
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 300,000 hadi shilingi 500,000 kwa mwezi.
Rais Dkt. Mwinyi ametangaza ongezeko hilo la mshahara leo, tarehe 01 Mei 2026, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi, na itaendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kukabiliana na changamoto zote zinazowakabili wafanyakazi hapa nchini.
Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imepata mafanikio makubwa tangu ilipoingia madarakani mwaka 2020, kwa kufanikiwa kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kupitia kurekebisha na kuongeza mishahara, kufanya mapitio ya posho na marupurupu ya watumishi, pamoja na kuimarisha mafao ya hifadhi ya jamii na kuanzisha mfuko wa bima ya afya kwa wafanyakazi wote pamoja na familia zao.
Amepongeza dhana ya utatu inayoendelezwa baina ya Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (ZATUC), na Chama cha Waajiri Zanzibar (ZANEMA) kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafanyakazi na waajiri kwa ujumla, ambapo changamoto 24 kati ya 29 tayari zimepatiwa ufumbuzi.
Rais Dkt. Mwinyi ametangaza kuwa Serikali imetenga nafasi za ajira 7,500 katika mwaka wa fedha 2026–2027, pamoja na kuendelea kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa vyama vya wafanyakazi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafanyakazi, na kuwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii, uzalendo, na kutanguliza maslahi ya umma.









Comments
Post a Comment