RAIS DKT. MWINYI AISHUKURU INDIA KWA MIRADI MIKUBWA YA MAJI ZANZIBAR


                                         Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru India kwa kuendeleza ushirikiano na misaada yake kwa Zanzibar katika sekta mbalimbali za maendeleo, kijamii na kiuchumi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Mei 2026, alipokutana na Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar, Balozi Kumar Praveen, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Balozi Mdogo wa India anayemaliza muda wake Zanzibar, Kumar Praveen._

Rais Dkt. Mwinyi amesema mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na India hapa nchini umekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha upatikanaji wa maji katika maeneo mengi ya mijini, na ameishukuru nchi hiyo kwa mafanikio hayo pamoja na kusisitiza kufanikishwa na kuendelezwa kwa mradi mpya wa takriban dola milioni 35 katika sekta ya maji.

Mradi huo mpya utatekelezwa kupitia uendelezaji wa skim tisa za maji, uwekaji wa matanki mapya, uchimbaji wa visima, ujenzi wa mtandao wa usambazaji wa mabomba Unguja na Pemba pamoja na ujenzi wa jengo la afisi ya mradi huo.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Balozi Mdogo wa India aliyepo Zanzibar, Kumar Praveen, alipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini, tarehe 14 Mei 2026._

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesifu mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana kupitia Chuo cha IIT Madras kilichopo Zanzibar katika kutoa mafunzo na kuleta mageuzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Ameishukuru India kwa kutoa fursa za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wananchi wa Zanzibar katika sekta mbalimbali, huku akisisitiza kuendelezwa kwa fursa hizo kwa ajili ya kujenga uwezo wa rasilimali watu hapa nchini.

_Balozi Mdogo wa India anayemaliza muda wake Zanzibar, Kumar Praveen, akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo alipokwenda kuaga, Ikulu Zanzibar._

Akizungumzia sekta ya afya, Rais Dkt. Mwinyi ameitaka India kuendeleza misaada katika sekta hiyo pamoja na taasisi za afya za nchi hiyo kuendelea kutoa huduma na mafunzo kwa watendaji na madaktari nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuridhika na uwekezaji unaofanywa na taasisi za sekta binafsi za India zilizowekeza Zanzibar katika miradi ya umeme mbadala, kwani inachangia juhudi za Serikali za kuwa na umeme wa kujitegemea.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mdogo wa India anayemaliza muda wake, Kumar Praveen, alipofika Ikulu Zanzibar kumuaga.._

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza umuhimu wa kuendelezwa kwa masuala ya utamaduni baina ya India na Zanzibar kutokana na ushirikiano uliopo kwa miaka mingi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Rais Dkt. Mwinyi amempongeza Balozi Praveen kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kuimarisha uhusiano baina ya Zanzibar na India, na kumtakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiagana na Balozi Mdogo wa India anayemaliza muda wake, Kumar Praveen, Ikulu Zanzibar._

Naye Balozi Kumar Praveen ameihakikishia Zanzibar ushirikiano zaidi, huku akisifu mabadiliko ya kasi na maendeleo makubwa yanayofikiwa na Zanzibar hivi sasa, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na hospitali, pamoja na kuahidi kuwa India itaendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA