RAIS DKT. MWINYI AHAIDI KIBALI AJIRA MPYA SEKTA AFYA


                                       Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inakusudia kutoa kibali cha ajira mpya katika mwaka mpya wa fedha kwa sekta ya afya na kada nyengine ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa wauguzi hapa nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 12 Mei 2026, katika Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Wauguzi lililoambatana na Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, hafla iliyofanyika Hoteli ya Verde, Mkoa wa Mjini Magharibi.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Wauguzi pamoja na viongozi mbalimbali katika Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Wauguzi lililoambatana na Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, katika Hoteli ya Verde, Mkoa wa Mjini Magharibi, 12 Mei, 2026._

Amewataka wauguzi, licha ya tatizo la uhaba wa wauguzi, kuwa wastahamilivu na kutokata tamaa, pamoja na kuendelea kufanya kazi kwa moyo, weledi na kuzingatia misingi ya kada hiyo muhimu katika sekta ya afya.

_Baadhi ya Wauguzi pamoja na viongozi mbalimbali wakifuatilia Kongamano hilo la wanza la Kisayansi la Wauguzi lililoambatana na Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani.._

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza mafanikio yaliyopatikana kitaaluma katika miaka 62 ya Mapinduzi, ambapo wauguzi wamepanda kutoka ngazi ya kawaida ya stashahada hadi kufikia ngazi ya uzamivu.

Amesema mchango wa wauguzi unazidi kuwa na thamani kutokana na mabadiliko ya teknolojia na changamoto mpya za kiafya.

Amelielezea kongamano hilo la kisayansi kuwa ni fursa na jukwaa muhimu la kujifunza mbinu mpya za kitaaluma na kuimarisha tafiti zitakazochangia utoaji wa huduma bora za afya.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali, kupitia Wizara ya Afya, itakabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya afya, hususan upungufu wa wauguzi na madaktari nchini.

Aidha, amewaomba washirika wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na changamoto za kiafya na kuimarisha rasilimali pamoja na nguvu kazi kupitia mafunzo na uimarishaji wa miundombinu ya sekta ya afya, ikiwemo ujenzi wa hospitali na upatikanaji wa vifaa

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa zawadi ya tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wauguzi Zanzibar (ZANA), Ndugu Aziza Ahmed, katika Kongamano hilo._

Amefahamisha kuwa wakati Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali Mpya ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Saratani Binguni, pia itahakikisha ujenzi huo unaenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kisasa ili kukidhi mahitaji ya hospitali za kisasa.

Akizungumzia suala la mafunzo kwa wauguzi, amesema Serikali italifanyia kazi suala hilo ili kuwa na sera nzuri ya mafunzo itakayohakikisha kila kada katika sekta ya afya inapatiwa mafunzo kwa utaratibu bora unaowezesha watendaji kujifunza na kujiendeleza kitaaluma.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa katika Kongamano hilo._

Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wauguzi kufanya kazi kwa moyo na huruma, kutoa huduma bora kwa wagonjwa bila ubaguzi, kuwa na kauli nzuri, ucheshi, pamoja na kuzingatia maadili ya kada hiyo.

Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani mwaka 2026 yameadhimishwa chini ya kauli mbiu isemayo: “Kuwawezesha Wauguzi ni Kuokoa Maisha” (Empowering Nurses, Saving Lives).

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA