MELI YA KWANZA YA KIMATAIFA YASHUSHA SHEHENA YA MAFUTA BANDARI JUMUISHI, MANGAPWANI ZAANZIBAR
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MELI ya kwanza kubwa ya mafuta ya Kimataifa kutoka Saudi Arabia yenye jumla ya lita Milioni 36 za mafuta ya ndege, petroli na dizeli yamewasili katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani, Zanzibar.
Kuwasili kwa meli hiyo moja kwa moja toka nje ya nchi, sasa kunaiondolea Zanzibar utegemezi wa mafuta yaliyokuwa yakishushwa bandari ya Tanga na kuletwa na meli ndogo Zanzibar jambo ambalo pia lilikuwa linaiongezea gharama ya uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Akizungumza kuhusiana na kuwasili kwa shehena hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph Kirangi alisema kuwasili kwa meli hiyo na kushusha mafuta moja kwa moja Zanzibar ni kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya uhifadhi wa raslimali hiyo muhimu kwa uchumi wa Zanzibar.
Kirangi alisema kitambo Zanzibar ilikUwa na changamoto ya upungufu wa nishati ya mafuta kutokana na kuwa na mahitaji makubwa kuliko upatikanaji wake na ilikuwa inategemea msambazaji mmoja kutoka Tanga.
"Kulikuwa na upungufu na uliongezeka zaidi kutokana na vita Mashariki ya Kati ya Iran, Marekani na Israel na tulikuwa na msambazajj mmoja kutoka Tanga ambaye kwa sasa mkataba wake umemalizika na tumeingia mkataba mwingine na Kampuni ya One Petroleum ambayo imeleta meli yake ya kwanza Zanzibar" alisema Kirangi.
Alibainisha kuwa meli hiyo imeleta kwa mara ya kwanza mafuta mengi kuliko kipindi chochote cha nyuma na kiasi hicho kinà ifanya Zanzibar kuwa na akiba ya mafuta ya takribani mwezi mzima.
Mara kadhaa na hata wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa bandari hiyo, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akieleza dhamira yake ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa na akiba ya kutosha ya mafuta na inajitosheleza kwa chakula kwa kuwa na ghala kubwa za kutosha katika bandari hiyo jumuishi na kununua nafaka kwa wingi wakati wa mavuno na kuhifadhi kwa ajili ya wananchi visiwa hivyo ili wavipate kwa bei stahiki hivyo kudhibiti mfumuko wa bei.




Comments
Post a Comment