MBETO: WANASIASA WASTAAFU WACHAMBUZI LINDENI MASLAHI YA TAIFA

                                          Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka viongozi wa siasa wastaafu, wanataaluma, wasomi wabobezi na wachambuzi  wa masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kutambua kuwa kubomoa Taifa ni rahisi kuliko kulijenga.

Pia ametaja kauli  au maneno yanapotolewa bila tafakuri ya kina mara nyingi  huzua sintofahamu na kusababisha uvunjifu wa amani.

 "Ukiichezea amani ni sawa na kuchezea upanga wenye makali   au  kuwasha moto kwenye nyasi kavu hivyo kusambaa na kuleta maafa makubwa" alisema Katibu wa Kamati Maalum ya NEC  Zanzibar, Idara ya Itikadi  Uenezi na Mafunzo , Khamis Mbeto Khamis.

Mwenezi huyo alisema kumezuka tabia za hivi karibuni za baadhi watu  kutamka maneno bila kupima athari na faida zake katika jamii yenye watu waungwana .

"Tabia ya baadhi  ya viongozi  Wastaafu kutoa maneno makali bila kuyapima ni hatari. Pia kuna  baadhi ya wasomi na  wanataaluma wanaoheshimika  hutamka maneno ya kuogofya. Wajue tu maneno makali hubomoa badala ya  kujenga nchi" alisema Mbeto

Katibu huyo Mwenezi  alisema ipo haja ya kujadiliana mambo kwa kufuata taratibu zinazofaa ambazo haziachi athari katika jamii lakini pia si uungwana watu wazima wakawa na sifa ya kusema sema hovyo kila uchao ili kutaka sifa ya utukufu.

Mbeto aliwataka Watanzania kujua thamani  ya  Umoja wao  kuliko hasara ya kutoa maneno yanayopandikiza chuki, hasama na uasi katika jamii.

"Wananchi,  wastaafu, wasomi, wachambuzi na wanataaluma  wanapaswa kuwa wa kwanza kuitakia mema Tanzania" alisema Mwenezi Mbeto.

Alibainisha kuwa watakao ifikisha Tanzania miaka mingine sitini Taifa likiwa moja ni watanzania wenyewe.

"Ni kosa mtu kufikiri yatakapozuka majanga  au machafuko ana uhakika wa kubaki salama. Fujo, ghasia na vurugu hazina macho wala masikio, huwadhuru matajiri, masikini, viongozi na raia wema  wasio na hatia bila kutarajia" alisema.

Aidha Katibu Mwenezi  huyo alisema hakuna  gumu lisiloweza kuzungumzika na kumalizwa kwa njia za kiungwana., hivyo  aliwashauri maneno yao yawe ya kulinda umoja wa Kitaifa.

"Wapo baadhi ya wenzetu wanataka kutumia fujo na  vurugu kama mtaji wa kushika madaraka. Huwezi kupata utawala kwa mbinu  hizo batili. Njia pekee  inayokubalika ni  demokrasia ya  uchaguzi  ili kushika uongozi badala ya kususia  " alisisitiza Mbeto.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA