MBETO: OMO MPOTOSHAJI, UCHAGUZI MKUU ZANZIBAR UMESHAPITA





Na Mwandishi Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi (CCM),  kimemtaka Mwenyekiti wa ACT Wazalendo  , Othman  Masuoud Othman   'OMO' kutowapotosha wananchi kwa kudai kuna waliojipa mamlaka wakati  kura zilizopigwa  ndizo zilizoiweka serikali  madarakani.

Katibu wa Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi na Uenezi, Komredi Khamis Mbeto Khamis alisema 
kwa muktadha huo, CCM  kimesikitishwa kumsikia kiongozi huyo  akipotosha  ukweli  kuhusu   Uchaguzi Mkuu uliopita.

Mbeto alisema kauli ya kiongozi huyo ni kama kwamba uchaguzi bado haujafanyika Zanzibar.

Mwenezi huyo alidai kuwa matamshi ya Mwenyekiti huyo   wa ACT Wazalendo yana    upungufu na  walakin.

"Wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya ACT  Wazalendo Jijini Dar es Salaam, Othman alidai kuna waliojipa madaraka huku wakishindwa kutenda  haki na  kutotimiza wajibu  stahiki kwa wananchi" alisema Komredi Mbeto. 

Alibainisha kuwa  hakuna Serikali  Duniani inayojiweka Madarakani bila  kupata ridhaa na idhini ya wananchi kupitia ushiriki wao katika demokrasia ya uchaguzi. 

Alisema jaribio la  kutaka  kuiaminisha jamii na Dunia ya kwamba Serikali iliyopo imejiweka madarakani ni upuuzi unaopaswa kupuuzwa.

"Hizo ni Ngenga , Varange na sarakasi za  kisiasa, jeuri na ukaidi usio na maana wala mantiki" alitanabaisha mwenezi huyo ambaye chama chake ndio kinaunda serikali.

Komredi Mbeto alisema ACT na CCM vyote vimeshiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Dunia nzima ikishuhudia na wagombea Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Vyama vyote waliomba kura wakapigiwa.

"Chama kilichoshinda kilitangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar hivyo ni makosa kudai kuna waliojiweka Madarakani"alisma Mbeto.

Katibu Mwenezi  huyo alisema CCM imekiita  kitendo cha Othman kupita akidai mshindi amejiweka madarakani,  madai hayo  ni porojo na pambio zisizo na uzito wowote .

"Wenzetu  kwa kutojua na  kutaka kuendekeza malumbano majukwaani wamekuwa  wakibeza maendeleo yanayofanyika ambayo wananchi kwa macho wanayaona mbaya zaidi bila wao kushiriki kutokana na kusua sua kwao  kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa" alisema na kuongeza kuwa bezo hizo zinawafanya wazidi kuporomoka kisiasa.

Mbeto alimtaka Othman akubali ukweli hakuwa na nguvu za kisiasa za  kumshinda mgombea Urais wa CCM, Dkt. Hussein Mwinyi,  ambaye tayari ameleta maendeleo  yaliyowaridhisha wananchi miaka mitano iliopita .

"Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 umeshafanyika na matokeo yametangazwa, kukaa na kudhani Uchaguzi Mkuu bado  haujafanyika ni kujidanganya mwenyewe. Uchaguzi umekwisha , mshindi amepatikana na ameshaunda serikali" alisema mwenezi Mbeto.






 




Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA