MBETO: DEMOKRASIA YA VYAMA VINGI 'ISILIPASUE' TAIFA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeviasa Vyama vya Upinzani na kuvitaka vielewe maana ya demokrasia ya Vyama Vingi si kuizuia Serikali isitimize wajibu wake au ihofie kuchukua hatua za Kisheria pale itakapobidi.
Kadhalika CCM kimeutaja ushindani wa kisiasa ikitaka uwe ni mchuano wa hoja na sera, si kukithiri matusi au kupandikiza hasama na chuki.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis, Zanzibar leo 11 Mei 2026.
Mbeto ambaye yuko katika Msafara wa ziara inayoendelea ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk Hussein Ali Mwinyi, alisema inashangaza kwa baadhi ya viongozi wa upinzani , wakisikika katika hotuba zao zikihamasisha hasama kwa lengo la kulipasua au kuligawa Taifa
"Ushindani wa siasa za chuki, hasama na matusi si kielelezo cha ustaarabu wa kisiasa. Tunawaonya wenzetu waache siasa zisizo na manufaa kwao, kwetu na kwa jamii yetu kwa ujumla" alisema Mbeto.
Pia Katibu Mwenezi huyo alisema tabia ya baadhi ya wanasiasa kutoa vitisho au madai yasio na ushahidi, hakuthibitishi kupevuka kwao badala yake wananchi huwapuuza.
"Huwezi kubagaza utu na heshima ya wenzako kisha uachwe ukitamba mitaani. Vyombo vya dola na vya kisheria vipo makini. Kutuhumu wenzako kwa masuala yasio na ushahidi si uungwana" alisema Mwenezi huyo.
Alibainisha kuwa siasa ni ushindani wa kimantiki unaoshindanisha hoja na sera, na inaeleweka kuwa kazi ya upinzani ni kufichua uovu ndani ya utawala lakini kuwe na ushahidi na vielelezo si kutamka matusi mbele ya jamii.
"CCM haijawahi kuhofia upinzani toka mwaka 1992. Walikuwepo kina Mabere Marando, Chifu Fundikira, Mapalala, Maalim Seif, Oscar Kambona na Mzee Mloo ambao hawakuwatusi watu, walitoa hoja na kujibiwa kwa nguvu ya hoja" alitanabaisha Komredi Mbeto.
Aliwataja waasisi hao wa mfumo wa vyama vingi na kubainisha kuwa walikuwa wamekomaa na wajenzi wa hoja makini na waliojua umuhimu wa amani na umoja bila kutoa vitisho au kueneza chuki za kisiasa.
Mbeto akirejea kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar kuhusu Serikali ya Ùmoja wa kiTaifa na mazungumzo ya kusaka muwafaka, alisema ipo wazi na ndio msimamo wa CCM kuwa ipo tayari kwa Serikali hiyo ambayo ipo kisheria kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar
Mwenezi huyo alienda mbali zaidi kwa kueleza kuwa kama kuna mazungumzo yatakuwa ni juu ya mambo yanayo husiana na Sheria iliyounda Serikali ya Umoja wa kiTaifa na kama kutakuwa na ambayo hayapo sawa, yatahitaji maamuzi ya mamlaka husika kama Baraza la Wàwakilishi na vyombo vingine vilivyowekwa na Katiba ya Zanzibar na Sheria zake.
"Huwezi kutaka mambo ambayo kwa mujibu wa Katiba yapo kwenye mamlaka ya Rais" alisema Mwenezi huyo.

Comments
Post a Comment