MBETO: CCM TUNAMPONGEZA DKT. MWINYI KUKATAA KUVUNJA KATIBA ILI ABAKI MADARAKANI ZANZIBAR

                                  Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza  uamuzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi  kwa  kushinda majaribu ya wapambe walioanza kumshinikiza avunje katiba  na  kuongeza muda wa kubaki  Madarakani Zanzibar.

CCM kimesema ni fedheha kwa wapambe na mashabiki walioanza kumshawishi kiongozi huyo abaki madarakani kinyume na Katiba ya CCM na ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu  wa Kamati  Maalum  ya NEC  idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo,  Khamis Mbeto Khamis kufuatia kauli ya Rais Dkt. Mwinyi aliyoitoa 22 Mei 2026 akifungua Mkutano wa Jukwaa la Watendaji Wakuu wa Taasisi la Zanzibar Chairpersons & CEO's Forum kuwa anasikia mjadala mitaani na kwenye Baraza la Wawakilishi wakimtaka aongeze muda wake madarakani jambo ambalo amelikemea na kutaka mjadala huo ukome kwani hauna tija.

Alibainisha Dkt. Mwinyi kuwa aliapa kuilinda Katiba ya Zanzibar hivyo hayupo tayari kuifanya vingine na kuhoji kusudio la hao wanaotaka aongoze muda kinyume na Katiba ya Zanzibar.

Mwenezi Mbeto alisema huo ndio uamuzi na msimamo wa CCM kuwa kwa mujibu wa Mila na  Utamaduni  wa CCM,  matakwa ya Katiba  ya Zanzibar ya mwaka 1984  na Katiba ya CCM, Rais atakaa madarakani vipindi viwili kwa miaka kumi na hatawania tena nafasi hiyo. 

Alisema matamshi yaliotamkwa na baadhi ya wapambe kwa utashi wao binafsi ni dhamira batili, kwani hakuna Rais kupitia CCM anayeweza  kupata nafasi ya kuongeza muda wa kubaki madarakani kinyume na taratibu. 

"Hata iweje kwa Rais aliye Madarakani  akitokea ameleta maajabu ya kiutendaji  katika kusimamia  maendeleo, muda wake  kikatiba utabaki kuwa ule ule wa miaka kumi madarakani. Kila Rais akimaliza miaka hiyo atawapisha  wengine" alisema Mbeto. 

Katibu Mwenezi huyo aliliita tangazo la Rais Dkt.  Mwinyi kukataa kubaki Ikulu ifikapo mwaka 2030 na kwamba hana fikra wala mpango  wa kuongeza muda ili abaki  madarakani ni aibu kwa walioanza kumshabikia.  

"Kiongozi  yeyote muungwana uheshimu Katiba aidha ya chama au nchi. Kuvunja  ahadi na miadi au kufanya kinyume chake hiyo ni  dalili ya kiongozi huyo kukosa utu na ustaarabu" alisisitiza.

Mbeto alisema Tanzania hususan ndani ya CCM, kuna  wanachama  wengi wenye uwezo wa kubeba dhamana ya Urais na kuitumikia nchi kwa uzalendo, uadilifu na uaminifu,  hivyo  nafasi ya  kiongozi  mmoja kubaki madarakani milele haipo.

"Nafasi zaidi ya miaka mitano ilitolewa kwa Waasisi  Wetu  Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume. Baada ya wao hatatokea yeyote wa kuongeza  muda zaidi ya kuongoza aidha kwa Zanzibar au kwa Tanzania" alieleza Mwenezi  Mbeto.

Comments