MBETO: ACT WAKIKATAA SERIKALI UMOJA WA KITAIFA HATUWEZI KUWALAZIMISHA


                                            Na Mwandishi Wetu, Pemba

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimebainisha kuwa hakiwezi kuilazimisha ACT Wazalendo kupeleka jina la Makamu wa Kwanza na ya Mawaziri wanne ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ili kuwatumikia wananchi na badala yake CCM kupitia Serikali yale itaendelea kufanya hivyo hadi watakapoungana nao kuwaletea maendeleo waliowapigia kura.


Katibu wa Kamati Maalum (NEC) Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema SUK ni takwa la Katiba na inaundwa kulingana na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar.

Alisema chini ya Sheria hiyo, chama kinachopata kuanzia asilimia 10 kinatoa Makamu wa Rais na idadi ya nafasi za Mawaziri inategemea idadi  ya Viti vya Uwakilishi walivyoshinda kwenye majimbo.

Kulingana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2025, CCM kilishinda kwa asilimia 74.8 na ACT Wazalendo asilimia 23.22 inayowapa Umakamu wa Kwanza wa Rais na Mawaziri wanne ambao Wizara zao zimetajwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Viwanda na Maendeleo ya Biashara, Afya na Wizara ya Utalii na Mambo Kale ambazo hadi sasa zimekaimiwa na Mawaziri kutoka CCM wakati Serikali inasubiri majina kutoka ACT Wazalendo.

Akizungumza na wanahabari akiwa Mkoa wa Kusini Pemba, mara baada ya hitimisho la ziara Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dkt. Mwinyi kuwashukuru viongozi na wanachama wa chama hicho, Mbeto alisema Serikali hiyo ni kwa Mujibu wa Katiba ambayo Rais Dkt. Mwinyi aliapa kuilinda.

"Uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ipo kikatiba na imeelekeza maeneo yake hivyo, mazungumzo hayawezi kuwa nje ya Sheria inayounda Serikali hiyo na ikitokea ikawa hivyo litahitajika kwenda kwa mapana zaidi bila kuathiri Katiba ya Zanzibar:" alisema Mbeto.

Alibainisha kuwa licha ya maslahi ya Taifa pia ya CCM lazima yazingatiwe na chama kimeshatoa angalizo na CCM haipo tayari kuburuzwa katika jambo ambalo litahusu mamlaka ya Rais na kinachofanyika kwa sasa ni kuwatumikia wananchi na  kutimiza ahadi za wakati wa uchaguzi mkuu 2025.

"Tunaendelea kuwatumikia wananchi, kutatua shida zao na kama wasipokuja tutaendelea kuwahudumia" alisema Mbeto.

Mwenezi huyo alirejea 2015 wakati Rais wa Serikali ya Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM akiwa Dkt. Ali Mohamed Shein chama hicho kilisusia uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini wananchi waliendelea kuhudumiwa.

 "CCM tunaitaka sana  Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini hatuwezi kuwabembeleza" alisema Mbeto na kuongeza kuwa shughuli za kuwahudumia wananchi na kutatua kero zao zinaendelea.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA