KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA MAENDELEO MIRADI YA UWEKEZAJI BAGAMOYO

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uwekezaji katika Kongani ya Viwanda ya Bagamoyo baada ya kufanya matembezi na ukaguzi wa miradi inayosimamiwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) katika eneo la Bagamoyo Eco-Maritime City (BEMC), mkoani Pwani 30 Mei, 2026.

Ziara hiyo ililenga kufahamu hali ya uendelezaji wa eneo hilo la uwekezaji pamoja na kujionea maendeleo ya miradi mbalimbali ambayo tayari imeanza kutekelezwa ndani ya eneo hilo la kimkakati.

Bagamoyo Eco-Maritime City (BEMC) ilitangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali Na. 123 la tarehe 24 Mei 2013 na ina ukubwa wa hekta 9,800, ambapo hekta 887 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Mbegani. 

Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuimarisha uwekezaji, maendeleo ya viwanda na biashara nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt. Damasi Ndumbaro, alisema kamati imeridhishwa na hatua mbalimbali za maendeleo zinazofikiwa katika eneo hilo na kwamba uwekezaji unaoendelea ni ishara ya mafanikio ya juhudi za Serikali za kuvutia mitaji na kuharakisha maendeleo ya viwanda.

Dkt. Ndumbaro alisema miongoni mwa miradi iliyovutia kamati hiyo ni Kiwanda cha nguo cha Sinovet.

Alisema mradi huo una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa za ajira kwa zaidi ya vijana 10,000, sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi, kuongeza kipato kwa wananchi wa Bagamoyo na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Dkt. Azizi Mlima, alisema mamlaka hiyo itaendelea kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zinazotokana na uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi, hususan katika maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.

Alisema uwekezaji unaendelea kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuongeza ajira, kuvutia mitaji, kuimarisha uzalishaji wa viwandani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa kamati, alisema Bagamoyo Eco-Maritime City ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha azma ya Tanzania ya kufikia uchumi wa dola Trilioni moja, kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa mwaka 2026/27–2030/31.

Teri alisema kuwa hadi kufikia tarehe 20 Mei 2026, jumla ya wawekezaji 24 walikuwa wamepatiwa maeneo ya uwekezaji na wameanza kutekeleza miradi yao katika hatua mbalimbali, ikiwemo kusawazisha maeneo, ujenzi wa uzio, mabanda ya viwanda (industrial sheds) pamoja na miundombinu ya msingi kama barabara.

Aliongeza kuwa maendeleo hayo yanaonesha kuongezeka kwa mwitikio wa wawekezaji katika eneo hilo na kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji yanayowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya viwanda na biashara.

Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ni sehemu ya jukumu lake la kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini na kutathmini mchango wake katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wananchi.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA