DKT MWINYI: WALIOHUSIKA UPOTEVU FEDHA ZA FIDIA WALIOPISHA MIRADI WAWAJIBIKE KABLA SERIKALI KUCHUKUA HATUA


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaunda Kamati Maalum ya Uratibu kufuatilia mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Tathmini ya Masuala ya Fidia kwa Wananchi waliopisha miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo 12 Mei 2026, alipokuwa akizungumza na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma baada ya kupokea ripoti ya Tume hiyo katika hafla iliyofanyika Ikulu, Zanzibar.

Ameeleza kuwa Kamati hiyo itafanya kazi zake kwa kipindi cha miezi mitatu (3) kufuatilia mapungufu na changamoto zilizobainika katika ripoti ya Tume ya Fidia, ikiwemo malipo yasiyostahiki, upotevu wa fedha na kumbukumbu za malipo ya fidia, walengwa kulipwa ziada, kucheleweshwa kwa fidia, pamoja na baadhi ya wananchi kutokuondoka katika maeneo husika licha ya kulipwa fedha stahiki, huku wengine wakiendeleza ujenzi baada ya kulipwa fidia zao.

Rais Dkt. Mwinyi amesema ni lazima watendaji na watu wote waliotajwa katika ripoti hiyo, na ambao hatimaye watathibitika kufanya udanganyifu na kuisababishia Serikali hasara kwa kupoteza fedha nyingi, wawajibike kabla Serikali haijawachukulia hatua za kisheria.



Aidha, amesisitiza kuwa fedha zote zilizopotea lazima zirejeshwe Serikalini.

Rais Dkt. Mwinyi ameielekeza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kulifanyia kazi suala la udanganyifu na upotevu wa fedha za umma kupitia fidia, pamoja na kupitia kumbukumbu zote za malipo zilizopotea ili kubaini wahusika na fedha ambazo zimebainika kutotumika kulipa fidia. Amesema watendaji wote waliohusika kupoteza kumbukumbu hizo wachukuliwe hatua za kisheria.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imepokea pendekezo lililotolewa na Tume ya Tathmini ya Fidia la kuundwa kwa Mfuko Maalum wa Fidia kwa ajili ya wananchi wanaostahiki kulipwa fidia wanapopisha miradi ya maendeleo, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti upotevu wa fedha za Serikali.

Ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuwa na mpango na muundo maalum wa aina ya majengo yatakayojengwa pembezoni mwa barabara, pamoja na kudhibiti ujenzi holela na matumizi mabaya ya njia za watembea kwa miguu katika barabara zote.

Dkt. Mwinyi pia ameagiza Tume ya Mipango Zanzibar kupitia kumbukumbu za fidia zilizolipwa kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo ili kubaini uhalali wake pamoja na watu waliolipwa. Aidha, ameiagiza Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ kupitia vikosi vyake kuwa na utaratibu maalum wa kulinda miundombinu ya miradi ya maendeleo kwa lengo la kuepusha hujuma zinazofanywa kwa makusudi.

Rais Dkt. Mwinyi amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Tathmini ya Masuala ya Fidia kwa Wananchi waliopisha miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini na kueleza kuwa ripoti hiyo ni miongoni mwa ripoti bora zilizowahi kuwasilishwa Serikalini.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA