DKT. MWINÝI: SERIKALI KUENDELEA KUTOA USHIRIKIANO IBADA ZA HIJJA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali kupitia Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana itaendelea kutoa ushirikiano katika kuimarisha huduma za Hijja na kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo mahujaji.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 03 Mei 2026, katika hafla ya kuwaaga mahujaji wanaokwenda kutekeleza Ibada ya Hijja Makkah, Saudi Arabia, iliyofanyika katika Msikiti wa Jamiu Zinjibar, Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi.
_Baadhi ya Mahujjaj wakimsikiliza, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, wakati wa hafla hiyo._
Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa safari ya Hijja ni muhimu kwa kila Muislamu, kwani ni utekelezaji wa Nguzo ya Tano ya Uislamu na kwamba mahujaji husafishwa nafsi zao na kuwa watu wema zaidi.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kumekuwa na mafanikio makubwa kila mwaka katika kukamilisha Ibada ya Hijja, hali inayochangia kuongezeka kwa idadi ya mahujaji na kuonesha mafanikio makubwa kwa Zanzibar.
_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akipokea zawadi maalum kutoka kwa Suleiman Masoud Makame, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, aliyemwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, katika hafla hiyo.
Alhaj Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia na mamlaka zinazotoa huduma za Hijja nchini humo, pamoja na Shirika la Ndege la Saudi Arabia na Ubalozi wa Tanzania nchini humo, kwa mchango wao mkubwa wa kuhakikisha mahujaji wa Zanzibar wanapata huduma bora na kwa urahisi wanapowasili.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesema Serikali itakamilisha hatua za kisheria ili Mfuko wa Hijja wa Zanzibar, ambao tayari umeanza kazi zake, uweze kuimarika na kuongeza idadi ya mahujaji wa Zanzibar kila mwaka.


.jpg)



Comments
Post a Comment