DKT MWINYI: CCM IPO TAYARI KWA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

                                        Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mazungumzo ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Chama cha ACT-Wazalendo yanaendelea, na kwamba CCM itasimamia ipasavyo maslahi ya Chama hicho pamoja na Taifa kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti, Dkt. Mwinyi, ameyasema hayo leo tarehe 09 Mei 2026 alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja katika mkutano wa kutoa shukrani baada ya Uchaguzi Mkuu, mkutano huo umefanyika katika Ofisi ya Chama hicho Mahonda.


Ameeleza kuwa CCM itaendelea kusimamia kwa umakini na busara mchakato huo, huku ikijielekeza katika kulinda na kuendeleza maslahi ya Chama na Taifa kwa ujumla, na kwamba CCM ipo tayari kushiriki katika kuunda Serikali hiyo.

Amesema ni vema viongozi na wanachama kujitathmini baada ya uchaguzi na kutobweteka, bali kujipanga kwa ajili ya Uchaguzi wa mwaka 2030 pamoja na uchaguzi wa ndani wa Chama hicho, sambamba na kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi wa mwaka 2025.

Dkt. Mwinyi, ameyataja mambo matano yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa lengo la kukiimarisha Chama hicho ambayo ni tathmini baada ya uchaguzi, umoja ndani ya Chama, maadili ya uongozi, utekelezaji wa Ilani pamoja na suala la uchumi ndani ya Chama, sambamba na kudumisha amani nchini.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani, amesema CCM imejipanga na inaendelea kufanya vizuri katika eneo hilo kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo, na kwamba itaendelea kutoa ahadi zinazotekelezeka huku akiwataka wanachama na wananchi kuendelea kukiamini Chama hicho.

Akizungumzia uchumi, Makamu Mwenyekiti, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema uchumi wa Zanzibar unaendelea kuimarika kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu ya bandari, tatizo alilolielezea kuwa lilikuwa changamoto kubwa kwa sekta ya usafiri na usafirishaji baharini.

Pia ametaja changamoto nyingine kuwa ni uhaba wa umeme na kueleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa umeme mbadala ikiwemo umeme wa jua, upepo na gesi asilia.


Kuhusiana na uchumi ndani ya Chama, Dkt. Mwinyi ameshauri kuwepo kwa vyanzo vya fedha ili Chama kiweze kujitegemea na kujiendesha kwa kutumia rasilimali zake pamoja na fursa za kiuchumi zilizopo, ikiwemo kuwa na maeneo mengi yanayoweza kufanyiwa miradi mbalimbali.






Kuhusiana na maadili ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa maadili bado yanalegalega na kutoa wito kwa viongozi na wanachama kuyashughulikia bila ya kumuonea mtu, sambamba na kuepukana na makundi ndani ya Chama.


Akihitimisha hotuba yake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza viongozi na wanachama wa CCM kujipanga vema kwa ajili ya kuimarisha uhai wa Chama hicho katika ngazi zote.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA