DKT. MWINYI: AWASHANGAA WANAOMTAKA AVUNJE KATIBA KWA KUONGEZA KIPINDI CHA URAIS ZANZIBAR
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapionduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi anasema anashangaa na haelewi sababu zao watu ambao wanamtaka avunje Katiba ya Zanzibar na aongeze kipindi cha uongozi wake madarakani.
Akizungumza 23 Mei 2026, wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma, Zanzibar Chairpersons & CEO’s Forum 2026, Rais Dkt. Mwinyi, ametaka mijadala hiyo ambayo inasikika mitaani na kwenye Baraza la Wawakilishi isitishwe mara moja.
“Hivi karibuni kumekuwa na mijadala sana kuhusu kuongeza kipindi cha uongozi, sijui sababu yake ni nini?, ndio kwanza tumeanza tuna miezi sita tu, maneno yamesha anza, Baraza la Wawakilishi nayasikia, mitaani nayasikia leo Kirobo (Msanii wa vichekesho) hapa anasema hayo hayo” alisema Dkt. Mwinyi.
Alibainisha kuwa yeye na wenzake wameapa kuilinda Katiba ya Zanzibar kwa hivyo hawataweza kufanya vinginevyo na kushangaa wasiwasi wa Urais unatokana na nini kwani bado kuna miaka minne na nusu ya kuwatumikia wananchi na baada ya hapo atakabidhi madaraka kwa mwingine.
“ Huu wasiwasi unatokana na nini? Mbona tuna miaka minne na nusu mizuri tu ya kufanyakazi, tumuombe mwenyezi Mungu uhai na uzima atuwezeshe kutekeleza majukumu yetu” alisema Rais Dkt. Miwnyi.
Alibainisha kuwa hana shaka kwamba na walipoanzia na mbele ya safari kutaendelezwa zaidi ili Zanzibar ipate maendeleo ambayo kila mmoja anayatarajia na kusisitiza kuwa mjadala huo si wakati wake kabisa na hauna nafasi.
“Kule Baraza la Wawakilishi kuna mambo mengi ya kujadili ya kimaendeleo, ni vema tukajadili hayo tuache jambo hili ambalo kwa kweli halina tija” alisema na kuwataka wasimamizi wa mashirika ya umma na taasisi zake zijipange kutoa gawio serikalini.
Rais Mwinyi ameyataka mashirika ya umma na taasisi za serikali zihakikishe zinafanya vizuri na kuondokana na ruzuku kutoka serikalini na yatapewa muda ili yajipange na yatakayoshindwa kufikia malengo, hakutakuwa na haja ya kuwa nayo.
“Hatuna haja ya kuwa na mashirika kama hayo ambayo yanainyonya serikali badala ya kuipa kulipa gawio serikalini” alisema Raisi Dkt. Mwinyi na kuongeza kuwa serikali itaendelea kusimia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

.jpg)







Comments
Post a Comment