DKT. MWINYI: TUMEANZA UJENZI NYUMBA 5,000 ZA WENYE MAKAZI CHAKAVU ZANZIBAR


Na Mwandishi Wetu, Pemba

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inakusudia kujenga nyumba 5,000 za makaazi kwa ajili ya wananchi wa Unguja na Pemba ndani ya miaka mitano.

_Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho Mkoa wa Kaskazini, Pemba katika Ukumbi wa Mikutano wa Wete, 13 Mei, 2026._

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo 13 Mei 2026, alipozungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Pemba katika mkutano maalum wa kutoa shukrani baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amefahamisha kuwa Serikali imeweka mkazo maalum katika ujenzi wa nyumba hizo za maendeleo ili kuwaondoa wananchi wanaoendelea kuishi katika nyumba chakavu na zisizo na ubora zinazohatarisha usalama wao.

_Baadhi ya wana CCM, wakimshangilia, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alipozungumza na viongozi na wanachama wa chama hicho Mkoa wa Kaskazini, Pemba katika Ukumbi wa Mikutano wa Wete, 13 Mei, 2026._

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema nyumba za zamani zilizojengwa zaidi ya miaka 62 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar hazifai tena kwa makazi, akizitaja nyumba za Michenzani, Bambi, Micheweni na Kilimani, huku akieleza kuwa ujenzi huo tayari umeanza katika nyumba za Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Makamu Mwenyekiti Dkt. Mwinyi amesema mradi huo wa nyumba 5,000 za makazi utatekelezwa na Shirika la Nyumba la Zanzibar baada ya Serikali kuliwezesha kuwa na uwezo mkubwa pamoja na utaalamu wa kutosha.

_Viongozi na wanachama wa chama hicho Mkoa wa Kaskazini, Pemba wakifuatilia mkutano huo katika Ukumbi wa Mikutano wa Wete, 13 Mei, 2026._

Dkt. Mwinyi amewahimiza wanachama kutimiza wajibu wao wa kukiimarisha Chama hicho kwa kuacha makundi ya uchaguzi katika kila ngazi, pamoja na kuhimiza kurejeshwa kwa madarasa ya itikadi kwa lengo la kuwaelimisha wanachama wajibu wao sambamba na kuingiza wanachama wapya.

Aidha, amehimiza Chama kuwa na uchumi imara kwa kuanzisha miradi mikubwa yenye tija kwa kutumia rasilimali za ndani za Chama Cha Mapinduzi katika kila wilaya na mkoa.

_Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akipokea zawadi maalum kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mzee Mberwa Hamad, mara baada ya mkutano huo wa kutoa shukrani kwa wanachama wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba.._

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amehitimisha ziara yake ya kutoa shukrani kwa wanachama baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, iliyoanza 09 Mei hadi 13 Mei 2026.

Ziara hiyo ilianza Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikifuatiwa na Mkoa wa Mjini Kichama, kisha kuendelea katika Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Magharibi Kichama kwa upande wa Unguja. Aidha, ziara hiyo imehitimishwa Kisiwani Pemba kwa kutembelea Mkoa wa Kusini Pemba na hatimaye Mkoa wa Kaskazini Pemba.


Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA