CCM YAIPONGEZA SMZ KUONGEZA KIMA CHA CHINI CHA MSHAHARA


                                     Na Mwandishi  wetu, Zanzibar  

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeipongeza kwa dhati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), chini ya Rais Dk Hussein Ali  Mwinyi kwa kupandisha mshahara kima cha chini kutoka TSh.300,000 hadi TSh.500,000 kwa mwezi.

CCM  kimeitaka SMZ  kuendelea mkakati wa kutazama hali za maslahi ya  wafanyakazi wa kima hicho ili waweze kustawi na kujijenga  kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Katibu  wa Kamati Maalum ya  NEC  Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis mara baada ya SMZ kutangaza kima kipya cha  mshahara wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, visiwani humo.

Mbeto alisema  ongezeko hilo la mshahara kwa kima cha chini ni fursa nyingine  kwa wafanyakazi  itakayosaidia katika kustawisha maisha yao.

Komredi Mbeto alisema mshahara huo mpya bila shaka SMZ imezingatia hali ya uchumi na maisha ya kila mZanzibari, gharama za maisha na kuwapa motisha wafanyakazi, wazidi kusimamia majukumu yao kwa ufanisi.

'Siku zote motisha huongeza tija kazini. Tunawahimiza  Wafanyakazi  wote katika  taasisi za umma,  Wizara, Idara na sekta zote wakasimamie nidhamu ya kazi ili kuongeza kasi ya uzalishaji" alisema Mbeto 

Aidha, alitoa kongole kwa uongozi wa SMZ Awamu ya Nane kwa kujali na  kutazama na kuinua hali za wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji ahadi  za kisera na  ahadi binafsi za Rais Dkt. Mwinyi.

"Tokea aingie madarakani Rais Dk Mwinyi hii ni mara ya pili kupandisha mshara kima cha chini. Anafanya haya yote kwa kujali watu na maisha yao. Uungwana  wa mtu ni kutenda si kusema maneno matupu" alibainisha Mbeto. 

Pia Mwenezi  huyo alisema CCM kitaendelea kuzishauri mara kwa mara serikali zake ili zihakikishe maisha ya wananchi yanakimbizana na hali halisi ya kiuchumi.

Comments