BAJETI KUU 2026/2027 NCHI ZOTE ZA E.A.C KUSOMWA PAMOJA
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar ameongoza ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaosimamia masuala ya Fedha na Uchumi, uliofanyika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, jijini Arusha.
Mawaziri hao wa Fedha na Uchumi kutoka nchi za Burundi, Congo, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudani Kusini na Uganda, pamoja na mambo mengine yanayohusu masuala ya utozaji wa pamoja wa ushuru wa forodha kwa Jumuiya hiyo, pia wamekubaliana kusoma kwa pamoja Bajeti Kuu za Serikali zao kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, hapo 11 Juni, 2026.
Katika Mkutano huo waliazimia pia kuwa na kaulimbiu ya utekelezaji wa Bajeti hizo, kaulimbiu inayodhamiria kuwezesha mtangamano na uhimilivu wa uchumi katika ukanda huo kwa kuwa na amani, matumizi ya kidijitali, na ufanisi katika makusanyo ya mapato ya ndani.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Pia Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Juma Mwenda, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursali Milanzi.
Wengine ni pamoja na Wataalamu wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, TRA, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).





Comments
Post a Comment