BALOZI OMAR AHUDHURIA UFUNGUZI MKUTANO WA MWAKA AfDB, CONGO BRAZZAVILLE
Na Mwandishi Wetu, Congo Brazzaville
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameshiriki halfa ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 61 wa mwaka 2026 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mkutano Mkuu wa 52 wa Mwaka wa Mfuko wa Maendeleo wa Benki hiyo (ADF), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kintélé, katika Jiji la Brazzaville, Jamhuri ya Kongo.
Katika ufunguzi huo, ujumbe wa Serikali ya Tanzania uliongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Mkutano huo wenye kauli mbiu ya "Kuhamasisha Ufadhili wa Maendeleo ya Afrika kwa Wingi katika Dunia Iliyogawanyika”, kauli ambayo inasisitiza umuhimu wa kuziba pengo la kifedha linalokua kwa mahitaji ya maendeleo ya Afrika, hasa katika mazingira ya kisiasa na kiuchumi duniani yanayobadilika kwa kasi.
Zaidi ya wajumbe 3,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na za mabara mengine ulimwenguni, zinashiriki mkutano huo, wakiwemo Marais na Wakuu wa Serikali za Afrika, Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu za nchi tofauti, washirika wa maendeleo, wawakilishi wa sekta binafsi, viongozi wa asasi za kiraia, wasomi, taasisi za utafiti, NGOs na wadau wengine wa maendeleo.
Upande wa Tanzania ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dkt. Hamad Omar Bakar, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali ambaye pia katika Muundo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika ni Gavana Mbadala wa Benki hiyo (Alternate Governor), Dkt. Natu El-maamry Mwamba.
Pia Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Rished Bade, Viongozi wengine kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.





Comments
Post a Comment