WAZIRI ATAKA NCHI ZA AFRIKA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI
WAZIRI wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Balozi Khamis Mussa Omar, amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuweka mipango ya kuhakikisha kuwa maji salama yanapatikana kwa ajili ya matumizi ya binadamu na shughuli za kiuchumi lakini pia kulinda vyanzo vya maji.
Balozi Omar alisema hayo wakati akichangia mada katika mkutano ulioangazia umuhimu wa sekta ya maji katika maendeleo ya watu na uchumi wa dunia, chini ya kauli mbiu “usalama wa maji kwa mustakabali wa bara la Afrika: mtazamo wa mbele” ulioandaliwa na Benki ya Dunia (WB), pembezoni mwa mikutano ya majira ya Kipupwe ya Benki hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) uliofanyika katika Jiji la Washington D.C, nchini Marekani.
“Pia ni muhimu kuvifuatilia na kuvilinda vyanzo hivyo na kuzitumia rasilimali hizo kwa uangalifu mkubwa ili tuendelee kuwa na maji safi, kuvilinda vyanzo hivyo dhidi ya uvamizi na uchafuzi wa maji, pamoja na kuondoa upotevu wa maji.” Alisema Balozi Omar.
Alitahadharisha kuwa idadi ya watu inaendelea kuongeza kwa kasi katila Bara la Afrika hatua inayosababisha kuwa na uhitaji mkubwa wa maji na kushauri kuwepo kwa ushirikiano madhubuti kati ya sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo kama WB ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili kutekeleza mira ya maji.
Mkutano huo wa maji uliwashirikisha mawaziri wa fedha na wadau wengine kutoka nchi wanachama wa benki hiyo katika baadhi ya nchi za Afrika na walijadili namna sera, uwekezaji, mabadiliko ya kimfumo wa kitaasisi unavyoweza kuboresha na kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama barani Afrika.




Comments
Post a Comment