UFUMBUZI CHANGAMOTO MUUNGANO KUTILIWA MKAZO
MAKAMJ Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali zote mbili za SMZ na SMT zitaendelea kuweka mkazo maalum katika kumaliza changamoto za Muungano ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi.
Amesema kuwa Serikali zitaendelea kufanya vikao na majadiliano kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto ambazo bado ni kikwazo kwa Muungano, aliouelezea kuwa wa kipekee duniani.
RaIs Dkt. Mwinyi, ameyasema hayo leo tarehe 26 Aprili 2026 katika kongamano la kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), lililofanyika katika Chuo cha Vijana Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amefahamisha kuwa miaka 62 ya Muungano imeleta mafanikio makubwa kwa pande zote mbili za Muungano katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi, na kuwasisitiza Watanzania kuuenzi na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya Taifa.
Makamu Mwenyekiti, Dkt. Mwinyi, amempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utayari wake wa kuendeleza dhamira na malengo ya Muungano kama ulivyoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1964, na kuendelezwa na viongozi wa awamu zilizofuata.
Dkt. Mwinyi amewahimiza Watanzania, hususan vijana, kuona umuhimu wa kulinda amani na kuepuka vishawishi vya uvunjifu wa amani, pamoja na kuudumisha Muungano ambao ni ngao muhimu ya umoja, mshikamano na udugu.
Aidha, amesisitiza kuwa Muungano una mchango mkubwa katika kuimarisha amani na utulivu wa nchi, huku akiwahakikishia kuwa Serikali zote mbili zitaendelea kuendeleza juhudi za kutatua changamoto zinazowakabili vijana nchini.
Ameeleza kuwa Serikali zote mbili chini ya usimamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeunda wizara maalum na kuweka mkazo mkubwa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana, pamoja na kutenga fedha maalum kwa ajili ya kuwawezesha kupitia fursa mbalimbali zilizopo nchini, ikiwemo ajira, nafasi za uongozi na kuboresha mitaala ya elimu ili vijana waweze kuajirika au kujiajiri.
Akihitimisha hotuba yake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa vijana kuendelea kutumia fursa zilizopo kisiasa, kijamii na kiuchumi, na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mambo yote aliyowaahidi wakati wa kampeni za uchaguzi.
Dkt. Mwinyi pia ameupongeza Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuona umuhimu wa kuandaa kongamano hilo la kuadhimisha miaka 62 ya Muungano, wakati huu ambapo nchi inaendelea kushuhudia mafanikio na maendeleo makubwa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, pamoja na kudumisha amani na utulivu.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akizungumza katika kongamano hilo la kuadhimisha miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, amewasisitiza vijana kuimarisha mshikamano kwani ndio nguzo muhimu ya kuimarika kwa Muungano, umoja na amani ya Taifa.
Kongamano hilo lilifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, sambamba na kufunga mafunzo ya uongozi na uzalendo kwa makatibu na wasaidizi makatibu wa UVCCM.






Comments
Post a Comment