TISEZA YAINGIA MKATABA UKODISHAJI ARDHI BAGAMOYO
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesaini mkataba wa upangishaji ardhi na kampuni ya HWTZ SEZ Limited kwa ajili ya ujenzi wa kongani kubwa ya viwanda katika eneo la Bagamoyo Eco Maritime City.
Akizungumza na waandishi wa habari 09 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri amesema mradi huo utatekelezwa katika eneo la hekta 500, sawa na asilimia 5 ya eneo la Bagamoyo SEZ, na ardhi hiyo imepangishwa kwa kipindi cha miaka 33.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo utahusisha ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo barabara, maji, umeme, pamoja na matumizi ya nishati jadidifu kama umeme wa jua. Pia, kabla ya mwisho wa mwaka 2026, viwanda vitatu vinatarajiwa kukamilika, ambavyo ni kiwanda cha kuunganisha magari, boti za uvuvi, kiwanda pikipiki, kiwanda cha vifaa vya ujenzi pamoja na kiwanda cha utengenezaji wa vipuri vya chuma.
Aidha, amesema mradi huo utagharimu takribani Dola za Kimarekani bilioni 3 na unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 5,000 za moja kwa moja kwa vijana pamoja na kuleta teknolojia za kisasa nchini. Kiwanda cha magari kitatumia nishati safi ya gesi asilia, hatua itakayochochea matumizi ya rasilimali za ndani na kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje.
Amesisitiza kuwa ardhi ya uwekezaji haiuzwi bali hupangishwa kwa mujibu wa sheria, huku kukiwa na vipengele maalum vinavyolenga kuhakikisha wawekezaji wanatekeleza walicho ahidi kufanya. Pia ametoa rai kwa watanzania kuwa fursa hii sio tu kwa wageni bali hata kwa wawekezaji wazawa wafike katika mamlaka ya TISEZA kuweza kupata vibali vya kuanzisha kongani za viwanda awe mtu binafsi au kwa kuungana na wengine watapewa kipaumbele.






Comments
Post a Comment