TANZANIA YAKARIBISHA UWEKEZAJI WA MAREKANI SEKTA MADINI, KILIMO, TEKNOLOJIA
Balozi Omar alieleza kuwa, Tanzania inaendelea kuimarika kiuchumi na kutoa mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji sambamba na uchumi wake kuendelea kukua kwa kasi, ukifikia asilimia 5.5 mwaka 2024 na unatarajiwa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2025, hali inayochochewa na sekta muhimu kama kilimo, viwanda, madini, ujenzi pamoja na huduma za kifedha.
“Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa muda mrefu ili kuhakikisha sekta binafsi inachukua nafasi yake kikamilifu katika kukuza uchumi” alisema, Balozi Omar.
Aliongeza kuwa mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Marekani yanaendelea kuimarika kwa kasi na thamani ya biashara kati ya nchi hizo imefikia Dola za Marekani Bilioni 1.4 mwaka 2024 huku uwekezaji wa moja kwa moja kutoka Marekani umeongezeka kutoka Dola Milioni 12.3 mwaka 2020 hadi Dola milioni 40 mwaka 2023.
“Hatupendelei kuuza mawe ghafi, bali tunakaribisha ushirikiano wa kuanzia uchimbaji hadi uzalishaji wa bidhaa za mwisho zenye thamani kubwa, na Tanzania ina soko kubwa la vijana wanaohitaji huduma za kidijitali, hivyo ni fursa adhimu kwa wawekezaji wa teknolojia pia,” alisema Balozi Omar.
Alibainisha kuwa katika sekta ya kilimo, Tanzania inalenga kuwa ghala la chakula kwa Afrika na Dunia, akihimiza uwekezaji katika kilimo cha kisasa na usindikaji wa mazao.
Pia alieleza kuwa sekta ya afya, miundombinu na maeneo maalum ya uwekezaji (SEZs) yana fursa kubwa kutokana na mahitaji makubwa ya soko la ndani na kikanda.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Sia Kanza alisema kuwa mkutano huo na wawekezaji wa Marekani ni jitihada za kuvutia zaidi mitaji kutoka Marekani kupitia Diplomasia ya kiuchumi.
Alisema kuwa Tanzania inaanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ambayo imeelekeza nchi iweze kufikia uchumi wa Dola za Marekani Trilioni 1 ifikapo Mwaka 2050 na kwamba uwekezaji wa Sekta Binafsi unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa.
Kwa upande wa wawekezaji walioshiriki mkutano huo ulioongozwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa BCIU, Peter Tichansky, alisema wameona kuna fursa za kiuchumi nchini Tanzania na wamejipanga kuwekeza katika sekta muhimu ikiwemo kilimo, madini, afya, miundombinu ya bandari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Bima ya wakulima.
Walisema kuwa eneo pamoja na maeneo hayo mengine, wanataka kuwekeza katika kilimo kwa kuzalisha mbegu bora pamoja na kuwawekea wakulima bima ya kilimo ili wawe na uhakika wa kuendesha shughuli zao bila kupata hasara ya majanga yatokanayo na changamoto mbalimbali.







Comments
Post a Comment