SAFARI ZA NDEGE MOJA KWA MOJA ZANZIBAR, ITALIA KUONGEZEKA JUNI 2026
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amemshukuru Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, kwa kuendelea kuimarisha na kupanua uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya Zanzibar na Italia, kwa kuzingatia ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 20 Aprili 2026, alipokutana na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo maalum, akiwa ameambatana na Balozi Mdogo wa Heshima wa Italia Zanzibar, Stephano Totisco.
___Rais Dkt. Mwinyi akisiitiza jambo wàkati wa mazungumzo yake na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola.
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kuongezeka kwa safari za Shirika la Ndege la Italia la NEOS kutoka tatu hadi kufikia tano kuanzia Juni 2026, ambapo shirika hilo linatarajiwa kuunganisha miji ya Bari na Catania na Zanzibar kupitia safari za moja kwa moja za ndege, kutaimarisha zaidi sekta ya utalii Zanzibar na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar.
Aidha, amesema Serikali imejikita katika kuboresha maeneo ya kihistoria yanayotumika kwa matamasha kama Ngome Kongwe, hivyo Zanzibar ipo tayari kuwa mwenyeji wa tamasha la muziki linaloandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania.
Tamasha hilo litawaleta wanamuziki wa asili na ngoma kutoka Italia, likilenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kitamaduni kati ya pande hizo mbili.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa mafanikio makubwa yanayoonekana Zanzibar, hususan katika uimarishaji wa miundombinu muhimu ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa barabara, shulei pamoja na masoko ya kisasa, hatua zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
___Rais Dkt. Mwinyi akipokea zawadi kutoka kwa balozi huyo wa Italia,Balozi Giuseppa Sean Coppola.___
Kuhusu sekta binafsi, Balozi Giuseppe Sean Coppola amesema kuwa Jukwaa la Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania (European Union–Tanzania Business Forum) linalotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam mwakani 2027, litakuwa na ajenda inayolenga zaidi kuendeleza sekta ya kilimo-biashara na mageuzi ya kidijitali, sambamba na maeneo mengine muhimu yenye maslahi ya pamoja.
___Rais Dkt. Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Giuseppe Sean Coppola (kushoto) ambaye aliambatana na Balozi Mdogo wa Heshima wa Italia Zanzibar, Stephano Totisco.___
Jukwaa hilo linatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi za pande zote, kukuza biashara na kuongeza ajira na thamani ya mazao.
_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiagana na mgeni wake mara baada ya mazungumzo yao._
_






Comments
Post a Comment