RAIS DKT. MWINYI: TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA WHO


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 09 Aprili 2026 alipokutana na ujumbe wa wataalamu kutoka Shirika la Afya Duniani, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Afrika, Profesa. Mohamed Yakub Janabi, waliowasili Ikulu Zanzibar.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na ujumbe wa wataalamu kutoka Shirika la Afya Duniani, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Yakub Janabi, katika mazungumzo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar._

Rais Dkt. Mwinyi amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na Zanzibar katika nyanja mbalimbali, ikiwemo mapambano dhidi ya malaria na kupunguza vifo vya kina mama na watoto, bado kuna haja ya kuungwa mkono na wadau, mashirika na taasisi za kimataifa, hususan kifedha, teknolojia pamoja na mafunzo kwa watendaji wa sekta ya afya.

Aidha, ameihakikishia WHO kuwa Serikali imekuwa ikifanya juhudi za makusudi kuhakikisha inaendelea kutumia rasilimali za ndani kukabiliana na changamoto za kiafya, huku ikiendelea kutafuta wadau na washirika wa maendeleo wa kimataifa ili kuimarisha sekta hiyo.

_Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Yakub Janabi, akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo._

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kudhibiti na kukabiliana na maradhi yasiyoambukiza (NCDs), kuimarisha afya ya uzazi kwa mama na mtoto, pamoja na kuwajengea uwezo wauguzi wa ngazi ya jamii kupitia mafunzo, ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya sekta ya afya.

Aidha, ameeleza kuridhishwa na misaada na mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ambao kwa kiasi kikubwa umechangia mafanikio yanayopatikana Zanzibar katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiagana Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Yakub Janabi, baada ya mazungumzo yao, Ikulu, Zanzibar._

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Profesa. Mohamed Yakub Janabi, amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya ili kufikia malengo na vipaumbele vyake, hususan katika kudhibiti maradhi mbalimbali.

Wataalamu hao wa WHO wamesifu hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuelekeza bajeti yake ya ndani katika kuimarisha sekta za afya, elimu na huduma za kijamii, wakieleza kuwa ni mfano bora kwa nchi nyingine nyingi za Kanda ya Afrika.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA