RAIS DKT. MWINYI: MISIKITI ITUMIKE KUTATUA CHANGAMOTO ZA KIJAMII


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza waumini wa dini ya Kiislamu kuitumia vema misikiti kwa ajili ya kujadiliana na kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo katika jamii.


Alhaj. Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 24 Aprili 2026, alipojumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyoambatana na ufunguzi wa Msikiti Mpya wa Jamaa Nour uliopo Boshowa, Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Ameeleza kuwa zipo changamoto nyingi katika jamii zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi, hususan zile wanazokabiliana nazo watu wa makundi maalumu, wakiwemo wajane, wazee wasiojiweza, watoto, watu wenye ulemavu na mayatima.


Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema waumini wana wajibu mkubwa wa kuitumia misikiti kusomesha dini, hususan kwa watoto ili waijue vema dini yao, pamoja na kusali kwa bidii na kumcha Mwenyezi Mungu, kwani hiyo ndiyo sababu kuu ya kujengwa misikiti mikubwa na mizuri katika maeneo mbalimbali.


Rais Alhaj Dkt. Mwinyi amewahimiza waumini kuutunza msikiti huo mpya ili ubaki katika haiba na mazingira bora wakati wote kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuchangia, pamoja na kuwatunza Maimamu na Walimu wa Madrasa, na kumshukuru mfadhili wa msikiti huo kwa uamuzi wake.




Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA