RAIS DKT. MWINYI ATAKA MABALOZI KUTANGAZA DIPLOMASIA YA KIUCHUMI UGHAIBUNI


                                          Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza mabalozi wanaoenda kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuweka kipaumbele katika kuzingatia diplomasia ya kiuchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo, 08 Aprili 2026, alipokutana na mabalozi hao waliofika Ikulu, Zanzibar, kumuaga kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi.

Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza mabalozi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili za Muungano, pamoja na kuweka kipaumbele katika utekelezaji wa sera kuu ya diplomasia ya uchumi.

_Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mabalozi waliofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha kabla ya kuelekea katika vituo vyao vya kazi, Aprili 08, 2026._

Aidha, amewaeleza mabalozi hao kuwa kwa upande wa Zanzibar, sera kuu ni Uchumi wa Buluu unaoambatana na utalii, hivyo ni vema wakaweka mkazo katika kuwashawishi wawekezaji kutoka mataifa hayo kuja kuwekeza nchini, kwani fursa zipo nyingi katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji.

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Zanzibar iko tayari kupokea wawekezaji, hususan katika uwekezaji wa miundombinu ikiwemo bandari, viwanja vya ndege, barabara, uvuvi na utalii.

Eneo jengine ambalo Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza ni upatikanaji wa wafanyabiashara na wawekezaji katika zao la mwani, pamoja na wale watakaowekeza katika ununuzi na uongezaji thamani wa zao la karafuu.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia mabalozi hao kuwa Serikali itaweka mfumo mzuri zaidi wa mawasiliano ili kuondoa urasimu kwa wawekezaji na kuongeza ufanisi. Aidha, amewapongeza na kuwatakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Balozi Swahiba Mndeme, akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao, amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa wameyapokea na watayatekeleza maelekezo yake kwa vitendo na kuitangaza kikamilifu diplomasia ya uchumi.

_Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mabalozi waliofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha kabla ya kuelekea katika vituo vyao vya kazi, Aprili 08, 2026. Picha zote na Ikulu, Zanzibar__

Mabalozi walioaga ni Balozi Mhandisi Zena Ahmed Said (Saudi Arabia), Balozi Cyprian John Luhemeja (Zambia), Balozi Maulidah Bwanaheri Hassan (Oman), Balozi Salim Othman Hamad (Comoros), Balozi Swahiba Habib Mndeme (Sweden), Balozi Noel Emmanuel Kaganda (Korea) na Balozi Mussa Haji Ali, Naibu Mwakilishi wa Kudumu Umoja wa Mataifa, New York.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA