RAIS DKT. MWINYI ASHUHUDIA SIMBA IKITWAA KOMBE LA MUUNGANO 2026


  Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewaongoza maelfu ya mashabiki wa soka kushuhudia mchezo wa fainali wa Ligi ya Muungano kati ya Simba na Yanga, uliochezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Timu ya Simba imefanikiwa kulitwaa kombe la michuano hiyo baada ya kuilaza Yanga 1-0, lililofungwa na mchezaji Selemani Mwalimu katika dakika ya 120 ya mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, kufuatia sare ya bila kufungana katika dakika 90 za kawaida.

Rais Dkt. Mwinyi, amelikabidhi kombe la ubingwa huo kwa nahodha wa Simba, Shomari Kapombe, pamoja na Hundi ya TSh. Milioni 150.

Pia Rais Dkt. Mwinyi, amekabidhi Hundi yenye thamani ya TSh. Milioni 100 kwa nahodha wa kikosi cha Yanga, Bakari Mwamnyeto, baada ya kuibuka washindi wa pili wa michuano hiyo iliyoandaliwa mahsusi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Timu nane zilishiriki michuano hiyo; nne kutoka Zanzibar ambazo ni Muembe Makumbi, Mlandege, KVZ na Mafunzo, na nne kutoka Tanzania Bara ambazo ni Simba Sports Club, Singida Big Stars, Azam FC na Young Africans.

Yanga ndiyo waliokuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo baada ya kulitwaa mwaka jana kwa kuilaza Azam FC katika mchezo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Gombani, Chakechake, Pemba.

Mchezo wa fainali ya Ligi ya Muungano ya mwaka 2026 umeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuwaenzi waasisi wa Muungano, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.


1.

2.
3

4.



Comments