MCHAKATO FIDIA WAKAMILIKA WALIOPISHA BARABARA KUSINI PEMBA
Na Mwandishi Wetu, Pemba
WAKAZI WA Chwaka na Ziwani, Mkoa wa Kusini Pemba ambao nyumba zao 36 zimevunjwa kupisha barabara, wameahidiwa kulipwa fidia zao hivi karibuni baada ya mchakato wa uthamini kukamilika na kuwasilishwa Hazina.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yake iliyoanzia Kusini Unguja na kumalizikia Chwaka, Mkoa wa Kusini Pemba, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, alisema kinachosubiriwa ni fedha kutoka hazina.
Makamu huyo wa pili wa Rais alisema kuwa wananchi waliopisha barabara zinazojengwa katika eneo hilo wanastahili fidia na ripoti imepelekwa Wizara ya Fedha ili waweze haki zao kwa mujibu wa sheria.
“Niwaambieni wananchi wa Chwaka fidia zitakamilika ndani ya kipindi kifupi kijacho, Kiwani tukasema, waliokuwepo wanasikia, kabla hatujamaliza Ramadhani mambo yakawa safi” alisema Makamu wa Pili.
Aliwataka wananchi hao kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na ndani ya kipindi kifupi barabara zote eneo hilo zitakuwa na lami na licha ya barabara pia kuna mambo mengine serikali imefanya.
“Tuliuwa na changamoto watoto Chwaka wanaenda kusoma Mtangazi sasa wanasoma hapo, hapo” alisema na kuongeza kuwa wahisani wa Save the Children pia wanajenga jengo la shule ya sekondari la ghorofa mbili, litakuwa na madarasa nane pia ametaka soko jipya la Kengeja kutumika ipasavyo na kutunzwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Badriya Atai Masoud alisifu kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi na msaidizi wake, Makamu wa pili Hemed.
Naibu waziri huyo alisema Jimbo la Ziwani lilikuwa na mahitaji ya barabara saba na tano tayari zimejengwa na zingine katika hatua tofauti.
“Barabara Wete-Chake Kilometa zaidi ya 25 na kati ya hizo sita zinapita Jimbo la Ziwani" alisema Naibu Waziri Badriya.
Alisema kuna nyumba takribani 39 zinazohitajika kulipwa fidia na kubainisha kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa miradi ya kimkakati hivyo anawaomba wananchi inapotokea mradi wawe wavumilivu kwani serikali haina dhamira ya kumdhulumu mtu yeyote katika suala la fidia isipokuwa kuna taratibu ambazo lazima zifuatwe ili fidia zilipwe.
Badriya alibainisha kuwa kuna miradi kadhaa inatekelezwa ya ujenzi wa barabara za lami ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kilometa 275.95, Pemba ikinufaika na kilometa 134.95 na Unguja kilometa 141
Pia katika mkataba wa kilometa 65.5 Pemba imepangiwa 40 na Unguja 25.5 pia mkataba wa 163.2, itajengewa kilometa 82.2 na Unguja ikipata 81.









Comments
Post a Comment