MBETO 'AMTOLEA UVIVU' KATIBU MKUU ACT WAZALENDO


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema  kabla ya muda wa madaraka kikatiba kumalizika Mwaka 2030, Serikali ya Rais  Dkt. Samia Suhuhu Hassan itawapatia Watanzania Katiba mpya.

Aidha chama hicho kimesisitiza hata Tume zilizokusanya maoni ya Wananchi za kina Jaji  Francis Nyalali ,Jaji Robert Kisanga na ile  ya  Jaji  Joseph Warioba, haikuwa ajenda ya upinzani.

Ufafanuzi huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum  ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis kufuatia madai ya  Katibu Mkuu wa ACT  Wazalendo,   Ado Shaibu aliyesema Katiba mpya  si agenda ya CCM. 

Mbeto alisema  Rais wa Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi  alikuwa  mwana CCM, Bunge la chama kimoja lilikuwa na Wabunge wa CCM pekee,  lakini kwa  kutojali maslahi ya kisiasa,  lilipitisha Sheria Namba 5 ya Vyama Vingi  Mwaka 1992.

Alisema hoja ya Katibu Mkuu huyo wa ACT ambaye pia ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini wakati  akiwa Bungeni, haikuzingatia ukweli wa historia wala  nia njema ya  Serikali  za CCM na  Wakuu wa Nchi.

"Ado ajenge hoja akiwa na rejea ya  ushahidi kamilifu Kudai kuwa hoja ya Katiba mpya si ya CCM huo  ni uzushi na  upotoshaji .Huenda wakati Sheria Namba 5 ya Mwaka 1992 ikipitishwa alikuwa anasoma shule ya Msingi" alisema Mbeto.

Rais Dk Samia mwaka jana  wakati akizindua kampeni za CCM  kwenye Viwanja vya Tanganyika Peckers jimbo la Kawe Jijini Dar es Salaa, aliwaahidi  waTanzania kabla ya kuondoka kwake madarakani kikatiba, Serikali yake itawapatia Katiba Mpya.

Pia Mbeto  alidai kuwa inawezekana Ado hajawahi kuziona wala  kuzisoma Ripoti za  Tume  ya Jaji  Nyalali na Jaji Robert Kisanga  ili kushuhudia  uamuzi  makini uliochukuliwa na Serilali ya CCM kuhusu vyama vingi.

"Wananchi Asilimia 80 walipendekeza  Mfumo wa chama kimoja uendelee. Asilimia 20 ndio  iliotaka Vyama vingi. Kudai ajenda ya Katiba mpya si ajenda ya CCM ni kukosa kwake ufahamu wa kutosha" alisema Komredi Mbeto. 

Mwenezi  huyo alibainisha kuwa laiti serikali na CCM, kingekuwa na ukiritimba kingelishikilia kuendelea na mfumo wa demokrasia ya chama kimoja kutokana na matakwa ya wengi.

Kadhalika Mbeto  alisema  hata kuundwa kwa Tume ya  kukusanya maoni ya Warioba,  baadae kuundwa Bunge Maalum la Katiba, yote hiyo ni kazi ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete hadi ikaandikwa  katiba pendekezwa.

"Mara kadhaa Rais  Dk Samia amewahi kusema  kwanza  anataka kujenga nchi. Hoja ya katiba mpya haifutiki wala kuchakaa. Katiba mpya bila shibe ,  maendeleo  na uchumi  imara haitabadili maisha yao" alisisistiza Mwenezi huyo.

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA