MBETO ABAINISHA DUNIA ISIVYO NA SHAKA NA DEMOKRASIA YA TANZANIA
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimejinasibu kuwa Tanzania inafuata na kutekeleza aina bora ya demokrasia chini ya uongozi wa chama hicho, kutokana na upana wake, ushiriki wa wananchi na uwazi usiotiliwa shaka.
Pia chama hicho kimesema kiwango cha ukosoaji, michango, fikra na maoni jumuishi ya wananchi husikilizwa, kutekelezwa na medani za utawala.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis aliposhiriki hitimisho la Mdahalo wa Muungano ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), kupitia Kigoda cha Taaluma cha Sheikh Abead Amani Karume.
Mbeto alisifu uwamuzi wa viongozi wa Mataifa ya Tanganyika na Zanzibar kwa kutanguliza kwao maslahi mapana ya Taifa kwa kuwaunganisha Wananchi miaka 62 iliopita.
Aidha alisema kiwango cha aina ya demokrasia iliopo nchini, kinatokana na ustawi wa uhuru wa wananchi.
Nafasi pana ya ukosoaji, utoaji maoni, ushauri huku wakipata maelezo toka serikalini.
Mbeto alisema ni nchi chache sana duniani zenye kufuata mfumo wa demokrasia inayolingana na utaratibu uliopo Tanzania
"Abadan sina shaka na aina ya demokrasia yetu Tanzania. Tuna ustawi mkubwa wa demokrasia iliovuka mipaka.
Leo kuna wanaofika hadi kutukana viongozi bila sababu hawakamatwi. Ni demokrasia yenye rutuba, kinga na Uvumilivu" alisema Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alisema ni nadra kuikuta aina ya demokrasia hiyo katika Mataifa mengine kama ilivyo Tanzania, lakini yote hiyo imetokana na dhima ya ukomavu wa kisiasa, uvumilivu, ujenzi mpya wa Taifa, mapatano na maridhiano.
Akijibu swali kuhusu msimamo wa chama chake wa kuandika katiba mpya, alisema kabla Rais Dk Samia Suluhu Hassan hajamaliza muda wake madarakani kikatiba, serikali yake itawapatia WaTanzania Katiba Mpya.
"Wakati Dkt. Samia alipokuwa akizindua kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa chama chetu katika Viwanja vya Tanganyika Peckers, amewaahidi WaTanzamia Serikali yake itawapatia Katiba mpya" alisema.
Kadhalika Mbeto alisema ajenda ya Katiba mpya ni ya Serikali za CCM, si ya upinzani. Tume zote za Ukusanyaji maoni ya wananchi zimeundwa na serikali zilizopo madarakani.
"Itaandikwa Katiba mpya itakayozingatia ushauri na maoni yote ya wananchi. Itapitia na kuzingatia mapendekezo ya Tume za Jaji Nyalali, Jaji Kisanga, Jaji Warioba na Jaji Chande" alisisitiza.
Hata hivyo, mwenezi huyo alisema Katiba mpya itafuata ushauri uliotolewa na wananchi, kulinda tunu za Taifa ustawi wa kisiasa, uboreshaji mifumo ya Uchaguzi na kuwashrikisha wadau wa maendeleo ya demokrasia.

Comments
Post a Comment