MAKAMU WA PILI WA RAIS ATAKA MKANDARASI PANGATUPU ASIONGEZWE MUDA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAKAMU wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdula ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko la Dagaa Pangatupu na kutaka muda zaidi usiongezwe kwa mkandarasi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kusini Unguja, Makamu alisema mkandarasi anapaswa amalize kazi katika muda huo wa nyongeza.
Makamu wa Rais alisema anaona ile azma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kutaka kuwe na mazingira mazuri kwa wavuvi inaenda kutimia ndani ya kipindi kifupi.
“Mhandisi Mshauri ametuelekeza vizuri, mradi unaendelea vizuri nami nakiri hatua niliyoikuta, mradi unaendelea vizuri na kwa kipindi ambacho wameongezewa muda wakamilishe kwa wakati” alisema.
Alibainisha kuwa kwa utaratibu wa serikali hivi sasa wakandarasi wakizidisha muda tunapendekeza waone gharama ya kuzidisha hivyo huwa wanatozwa na kuilipa serikali na wameongeza muda wasije wakaongeza tena kwa kuwa mradi unahitajiwa na waZanzibari walio wengi.
Alisema Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ana mipango mikubwa na sekta hiyo ya Uvuvi na ndio maana ameona umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya wavuvi na wadau wa sekta hiyo hasa mkoa wa kaskazini.
“Mkoa wa Kaskazini wengi wanajishughulisha na uvuvi na kwa kutambua umuhimu wake ndio maana awamu ya nane ikaanzishwa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ” alisema Makamu Hemed.
Alisema hatua iliyofikiwa ni kubwa kulinganisha na awali ambako wenyeji walianika dagaa chini na kuwataka wakazi wa eneo hilo kutambua kuwa dagaa ni biashara kubwa kwani pia kuna watu toka D.R Congo wanawafuata mkoani humo.
“Mambo mengi yamefanyika na makubwa zaidi yanatarajiwa kufanyika lengo likiwa kuweka mazingira mazuri kwa wavuvi na wadau wa uvuvi hasa mkoa huo wa Kaskazini” alisema na kuongeza kuwa hilo likifanyika vizuri jamii ya wavuvi itasaidika na sekta itatoa mchango katika kukuza uchumi wa nchi.
“Niwaambie, biashara ya dagaa ina faida kubwa sana, bado watu wanachukulia uvuvi ule tunaofanya kienyeji ikikamilika miradi hii ina maana wawekezaji watakuja na hata uvuvi utakuwa wa kisasa pamoja na hatua zote kwa miundombinu inayowekwa” alisema.
Makamu alibainisha kuwa anapata faraja kubwa kwani kuna wawekezaji wengi wanaotaka kuwekeza sekta ya uvuvi ambao wameanza kujitokeza baada ya kuona dhamira njema ya serikali na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ya kuboresha maeneo hayo ya pangatupu.
Makamu Hemed, alisema kuwa alipokuja kwa mara ya kwanza aliagiza wananchi walipwe fidia kuruhusu ujenzi wa mradi na amefurahi kusikia wote wamelipwa tayari na kuwahakikishia soko likikamilika, wote watafanya shughuli zao hapo hawajafukuzwa.
“ Shughuli zinazoendelea hapa watakuwa sehemu ya mradi na tutawazingatia kwa umuhimu wake na wajibadilishe kutokana na mazingira yalivyorekebishwa ili tuendane na hadhi ya masoko yanavyotakiwa duniani” alisema.
Pia alitanabaisha kuwa soko hilo linakwenda kusaidia upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo jirani kati ya zile 350,000 zinazotajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2025.





Comments
Post a Comment