MAKAMU WA PILI NA MAAGIZO MATATU KITUO CHA AFYA JADIDA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MAKAMU wa Pili wa Rais Hemed Abdulla Suleiman, ametoa maagizo matatu kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibnar (SMZ), mara baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Afya Jadida, kilichopo Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza katika ziara yake hiyo iliyoanzia Unguja ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali, Makamu wa Pili Hemed, alisema amekagua na kuona jengo limekamilika kwa kiasi kikubwa vifaa vingi vimeanza kufungwa.
Alibainisha kuwa hata kama mzigo umefika haa kama kifaa hakina kiwango urejesheni mzigo ulipotoka sababu tunapoagiza kifaa tunaweka viwango vyetu.
“Kama hakina kiwango hata kama kifaa kimefika, kirejesheni mzigo ulipotoka na huyo aliyeagiza atakirejesha na kuleta kingine kwa gharama zake na kwa mujibu wa ubora tuliokubaliana” alisema.
Jambo la pili alisema vifaa ni vya kisasa sana na anaamini vitahitaji madaktari kwani kuwa na jengo zuri si hoja, watu wanachohitaji ni huduma.
“Lazima tuhakikishe hapa wanapatikana madaktari wenye sifa na uwezo wa kufanyakazi kwa kadiri inavyowezekana kwa mujibu wa hadhi ya kituo hiki” alisema Makamu.
Alibainisha kuwa kulifungua jengo hili bila madaktari wanaostahiki litakuwa jambo halijaisaidia serikali wala wananchi tunaokusudia kuwapa huduma.
Makamu huyo alisema kuwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameshaelekeza kuwa madaktari wanapatikana na dawa zipo.
“Jambo la tatu ni huduma, nitawaomba sana wale ambao watakaopata bahati ya kuhudumia kituoni hapa na kituo kingine chochote wafanyekazi kwa bidii na weledi" alisema.
Alitaka maslahi na haki zao zisimamiwe na mwisho wa siku waweze kufanyakazi inavyostahiki.
'Najua madaktari mpo hapa inawezekana mkasema tunadai hiki, tunadai kile mtuambie tuwalipe, sisi serikali hatutaki kudaiwa, lazima niwaambie ukweli, serikali ya Rais Mwinyi haitaki kudaiwa" alisisitiza..
Aliwaambia kuwa changamoto kama hizo kukaa nazo bila kusema anapokuja Makamu kisha zinatajwa anapokuja Rais basi ni wazi kutakuwa na changamoto ya kiutendaji lazima hatua zitachukuliwa na hakutakuwa na mjadala mwingine.
"Mkamilishe jengo kwa haraka ili wananchi waweze kulitumia” alisema kuongeza kuwa kuwepo kwa zahanati hiyo, kutasaidia kupunguza usumbufu kwa wananchi ambao walikuwa wakiifuata huduma hiyo umbali mrefu na aliwashajihisha Bima ya Afya wakamilishe taratibu za kuwepo hapo kuhakikisha dawa zote stahiki zinapatikana hapo saa 24.



Comments
Post a Comment