DKT. MWINYI: WATANZANIA WANAWAJIBU KATIKA MUUNGANO


                                             Na Mwandishi Wetu, Pemba

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Watanzania wana wajibu wa kuhakikisha Muungano wa Tanzania, amani, utulivu na umoja wa kitaifa vinalindwa, vinaimarishwa na kudumishwa wakati wote.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 02 Aprili 2026, katika Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 uliofanyika katika Uwanja wa Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Rais, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akipoke nakala ya kitabu cha Miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na Mwongozo wake wa 2026, kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana Tanzania, Joel Arthur Nanauka, wakati wa uzinduzi wa mbio hizo.

 Pia amezitaka tasisi za dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wananchi wana wajibu wa kulinda misingi ya utu na kuheshimu utawala wa sheria ili kuwa na Taifa linalosimamia haki, usawa, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ni chombo muhimu cha kuhimiza haki, usawa, umoja na uwajibikaji katika ujenzi wa Taifa, sambamba na kuangaza na kutokomeza maadui wa maendeleo ambao ni umasikini, ujinga na maradhi, ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya viongozi waasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kisiasa na kijamii ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na utulivu wa nchi huwapa viongozi fursa ya kuandaa sera za maendeleo endelevu na kusimamia utekelezaji wake kwa ufanisi.

Amefahamisha kuwa ubaguzi kwa aina yoyote una matokeo mabaya na unaweza kusababisha hali ya kutoaminiana, utengano wa kikabila, kidini, kisiasa au kijiografia, na hatimaye kuingiza nchi katika misuguano inayoweza kupelekea machafuko na mgawanyiko mkubwa wa kitaifa.

Amewahimiza Watanzania kupinga aina zote za ubaguzi na kudumisha umoja wa kitaifa, kwani ni wakati sahihi wa kuonesha uzalendo kwa Taifa, kulinda rasilimali na kujenga kizazi kinachotanguliza mbele maslahi ya nchi.

Rais Dkt. Mwinyi amevinasihi vyama vya siasa na viongozi wake kutekeleza majukumu yao kwa kutanguliza Tanzania kwanza, pamoja na kuhakikisha tunu ya amani inalindwa wakati wote. 

Pia amewasisitiza wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na rushwa nchini na kuwa tayari kuwafichua wale wote wanaojihusisha na utoaji na upokeaji wa rushwa.


Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaendelea na juhudi za mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa za ARV bila malipo, pamoja na kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo hadi kufikia 24,000 katika mwaka 2024.

Kuhusiana na janga la dawa za kulevya, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali zote mbili zimeendelea kuimarisha operesheni katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege, pamoja na kutoa elimu hususan kwa vijana ili kupunguza matumizi ya dawa hizo.


Aamefahamisha kuwa hadi kufikia mwezi Desemba 2025, waraibu 18,970 walipatiwa huduma za tiba katika vituo 16 vya matibabu na zaidi ya waraibu 19,000 wanahudumiwa katika nyumba 77 za upataji nafuu.

Pia waraibu 728 walipatiwa huduma za tiba katika Kituo cha Tiba na Marekebisho ya Tabia cha Kidimni, Zanzibar.

Kuhusu ugonjwa wa malaria, Rais Dkt. Mwinyi amesema takwimu za Wizara ya Afya (SMT) za mwaka 2025 zinaonesha kuwa takriban asilimia 6.2 ya wagonjwa milioni 2.8 wa nje (OPD) walithibitika kuwa na malaria, na wagonjwa 199,347 waliolazwa hospitalini  na asilimia 11 walikuwa na malaria, wengi wao wakiwa watoto chini ya miaka mitano na mama wajawazito.

Rais Dkt. Mwinyi amesema pamoja na ugonjwa huo kuwa sugu, Serikali imepiga hatua kubwa katika kuudhibiti, ambapo hadi kufikia mwaka 2025 kiwango cha maambukizi kimepungua kutoka asilimia 8.1 mwaka 2022 hadi asilimia 5.5 mwaka 2025.

Amesema Serikali imechukua juhudi mbalimbali za kupambana na malaria, ikiwa ni pamoja na kusambaza vyandarua vyenye dawa, kudhibiti mazalia ya mbu, na kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu. 

Serikali pia imetenga TSh.Bilioni 10 kwa ajili ya kununua zaidi ya lita 833,000 za viuadudu vya kibaiolojia vilivyosambazwa katika halmashauri 184, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa vipimo na dawa unafikia zaidi ya asilimia 90 katika vituo vya afya.

Tayari Mwenge wa Uhuru umeanza kukimbizwa rasmi katika Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba, baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Hadid Rashid, kukabidhiwa Mwenge huo na Kiongozi wa Mbio za Mwenge kufuatia hafla ya uzinduzi.

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 zimebeba kaulimbiu isemayo: “TANZANIA NI YETU SOTE, TUSHIKAMANE".

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA