DKT. MWINYI: USONJI CHANGAMOTO KATIKA JAMII


                                     Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Hali ya Usonji kwa watoto ni changamoto kubwa katika jamii, hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha inaunga mkono jitihada za kuwasaidia watoto wanaoathirika na hali hiyo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo  20 Aprili 2026, alipokutana na viongozi wa Lukiza Autism Foundation waliomtembelea Ikulu kujitambulisha na kueleza shughuli za taasisi hiyo.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Lukiza Autism Foundation, walipomtembelea Ikulu Zanzibar, tarehe 20 Aprili, 2026._

Dkt. Mwinyi amesema kuwa tatizo la Usonji limekuwa changamoto kwa wananchi wengi, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha kwa jamii pamoja na uhaba wa wataalamu wa fani hiyo.

Ameeleza kuwa Serikali itachukua hatua za makusudi kuhakikisha wataalamu wanapatikana ili kutoa elimu kwa wananchi, pamoja na kuanzisha programu za uelimishaji mashuleni kwa lengo la kuongeza uelewa na kusaidia watoto wenye Usonji.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na viongozi hao._

Aidha, Dkt. Mwinyi ameigiza Wizara ya Afya kushirikiana na wataalamu hao ili kujifunza zaidi kuhusu Hali ya Usonji, akibainisha kuwa kwa sasa Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa kutambua na kushughulikia hali hiyo mapema.

Amesisitiza pia kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha uelewa wa Hali ya Usonji unaongezeka na huduma bora zinapatikana kwa watoto wanaoathirika.

_Mtendaji Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe akielezea jambo wakati wa mazungumzo hayo._

Mtendaji Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe, amesema kuwa bado Zanzibar inakabiliwa na changamoto nyingi katika kutambua watoto wenye Usonji kutokana na ukosefu wa wataalamu na vituo maalum vya huduma hiyo.

Amefafanua kuwa taasisi hiyo imejipanga kutoa elimu kwa jamii kwa ujumla, kuanzia ngazi ya familia hadi mashuleni ili kuongeza uelewa na kusaidia utambuzi wa mapema wa watoto wenye hali hiyo.

_RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akisikiliza maelezo kuhusiana na mfano wa jezi iliyochorwa kutoka kwa Mtendaji Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Lukiza Autism Foundation, Hilda Nkabe._

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa takribani watoto milioni 2 nchini Tanzania wanakadiriwa kuonyesha dalili za Usonji, huku kati yao watoto 14,000 hadi 20,000 wakionesha dalili zinazoweza kutambuliwa kuwa na hali hiyo.

_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Lukiza Autism Foundation. Picha Zote na Ikulu, Zanzibar_

Comments

Popular posts from this blog

CCM YAISHUKURU SMZ, WAKAZI KIKWAJUNI

CCM YAONYA WATEULE MIUNDOMBINU ZANZIBAR

TRA YATAKIWA IJIPANGE DIRA MAENDELEO YA TAIFA