DKT. MWINYI: TUNA KILA SABABU KUENDELEZA USHIRIKIANO NA IRELAND
Na Mwandishi Wetu, Zanziba
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar ina kila sababu ya kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu baina yake na Ireland.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 30 Aprili 2026, alipokutana na Balozi Nicola Brennan anayeiwakilisha Ireland nchini, aliyefika Ikulu, Zanzibar kwa mazungumzo maalum.
_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika mazungumzo na mgeni wake, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan, Ikulu Zanzibar._
Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Ireland kuwa Zanzibar itaendelea kuendeleza na kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na maendeleo, ustawi wa jamii, biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi hizo mbili rafiki.
Aidha, ameeleza kuwa uhusiano baina ya nchi hizo, ambao ni wa muda mrefu sasa, unapaswa kuelekezwa zaidi katika masuala ya uwekezaji na biashara kutokana na mahitaji, mwenendo na mabadiliko ya kiuchumi duniani.
_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika mazungumzo na mgeni wake, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Nicola Brennan na ujumbe wake, Ikulu Zanzibar._
Amefafanua kuwa Zanzibar imeweka mkazo madhubuti katika sekta za kipaumbele za uchumi wa buluu, utalii na uwekezaji.
Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Ireland kwa misaada inayotoa kwa Tanzania, ikiwemo katika nyanja za afya, elimu, ustawi wa jamii na mafunzo ya kuimarisha mfumo wa sheria hapa nchini na kuiomba kuendelea na misaada hiyo ambayo imekuwa ikichochea mabadiliko makubwa.
_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi, Nicola Brennan, Ikulu Zanzibar._
Aidha, amesema bado Zanzibar inahitaji wawekezaji zaidi na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Ireland, hususan sekta binafsi, kuja kuwekeza nchini katika sekta za utalii, uvuvi, biashara, uendelezaji wa kilimo cha mwani, miundombinu pamoja na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Akizungumzia Mji wa Urithi wa Mji Mkongwe, Rais Dkt. Mwinyi amesema ni eneo muhimu la kihistoria kwa Zanzibar na maendeleo ya sekta ya utalii, linalopaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi na washirika wa maendeleo, kwa kufanya kazi pamoja na Serikali ili kuhakikisha uhifadhi wake unakuwa endelevu.
_Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akiaga na mgeni wake, mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu Zanzibar._
Naye Balozi Nicola Brennan, ameihakikishia Zanzibar ushirikiano zaidi na nchi hiyo na kupongeza maendeleo makubwa yanayofikiwa katika sekta mbalimbali yanayochangia ukuaji wa uchumi, ujenzi wa miundombinu, ustawi wa jamii pamoja na kuimarika kwa amani na utulivu. Aidha, ameahidi fursa zaidi za mafunzo, hususan katika kada ya sheria hapa nchini.





Comments
Post a Comment