DKT. MWINYI: TUMEWEKA KIPAUMBELE KUIMARISHA KUHIFADHI MAENEO YA KIHISTORIA
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha na kuhifadhi maeneo ya kihistoria kwa kuzingatia umuhimu wake katika uchumi na uhifadhi wa utamaduni wa Zanzibar
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokutana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoet, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo maalum.
Akizungumzia hatua hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ukarabati mkubwa unaoendelea katika jengo la Sinema ya Majestic lililopo Vuga unafanyika chini ya ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Japan, ukiwa na lengo la kulibakisha katika muonekano wake wa asili na kulifanya kuwa endelevu.
Ameongeza kuwa kukamilika kwake kutachochea kufanyika kwa matamasha mbalimbali ndani ya jengo hilo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ina mipango endelevu ya uhifadhi wa majengo muhimu yenye historia ya muda mrefu, ambayo ni nyenzo muhimu katika kuitangaza Zanzibar na kuimarisha sekta ya utalii, kwani wageni wengi huyatembelea maeneo hayo wanapokuja nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Uholanzi kwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Tanzania, ikiwemo Zanzibar, katika nyanja mbalimbali pamoja na misaada inayotolewa katika kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.
Rais Dkt. Mwinyi pia amewakaribisha wawekezaji kutoka Uholanzi kuja kuwekeza nchini, hususan katika sekta za kipaumbele za utalii na uchumi wa buluu kwa ujumla. Amesema hatua hiyo itachochea ongezeko la watalii kutoka nchi hiyo na kubainisha kuwa Zanzibar bado inahitaji wawekezaji zaidi katika sekta za viwanda, uvuvi na kilimo.
Balozi wa Uholanzi, Marjo Crompvoet, ameihakikishia Zanzibar kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano pamoja na misaada katika sekta mbalimbali.
Ameeleza kufarijika na hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi yanayofikiwa na Zanzibar, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali, huku akiahidi ongezeko la wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kuwekeza Zanzibar.
Wakati huohuo, Rais Dkt. Mwinyi amekutana na Balozi wa Slovakia nchini, Bw. Ivan Lančarič, aliyefika Ikulu kujitambulisha, akiambatana na Balozi Mdogo wa Slovakia ambaye kituo chake rasmi kitakuwa Zanzibar, Mustafa Khataw.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi ameihakikishia Slovakia kuwa Zanzibar iko tayari kufungua milango ya ushirikiano na kufanya kazi na nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, uwekezaji, biashara na utalii, pamoja na kuishauri kuitangaza Zanzibar katika soko la utalii la nchi hiyo.
Naye Balozi Ivan Lančarič amesema nchi hiyo inatarajia kufungua ofisi ya ubalozi wake nchini Tanzania mapema mwezi Juni mwaka huu, hatua itakayokwenda sambamba na ufunguzi wa ofisi ndogo ya ubalozi wake Zanzibar, kwa lengo la kuendeleza ushirikiano.
Alisema, Slovakia ina maendeleo makubwa katika uchumi wa viwanda, teknolojia ya utengenezaji wa magari, pamoja na biashara na uwekezaji.




Comments
Post a Comment